Vipo vishawishi vingi sana vya kukufanya umkosee Mungu wako.

Vishawishi ambavyo vinavutia sana kwa macho na kwa maneno yake ukiyasikiliza.

Utakavyovitambua vishawishi hivyo nia yake ni ili umkosee Mungu wako, au umtende dhambi Mungu wako.

Hupaswi kukubaliana na mtu yeyote, bila kujalisha ni nani amekuambia ufanye hicho anachokuambia.

Anaweza akawa mtu wako wa karibu sana, ukaribu wenu usikufanye ukamkosea Mungu wako.

Unajua kabisa kufanya jambo fulani ni dhambi, usiangalie aliyekuambia fanya ni mzazi wako, ama ni mtoto wako, ama ni mke/mume wako.

Angalia kile ambacho Mungu anasema usifanye, wala usije ukajaribu kulifanya lile alilokukataza Mungu.

Hili lipo kibiblia kabisa, usije ukamsikiliza mtu anavyokushawishi ukamkosea Mungu wako.

Rejea: Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako; usimkubalie wala usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche; KUM. 13:6‭, ‬8 SUV.

Usije ukasahau hili na ukamwonea mtu huruma anapokushawishi kufanya jambo lilokinyume na neno la Mungu.

Mume wako anakuambia tungefanya hivi mke wangu ingependeza sana, alafu wewe ukiangalia analokuambia unajua kabisa ni kosa mbele za Mungu kulifanya hilo.

Mzazi wako anakuambia mwanangu ni vizuri kuheshimu ibada za kimila, alafu ukiangalia neno la Mungu linakuzuia kuabudu miungu mingine.

Usije ukaleta ukawaida na kusema haina shida, utakuwa umefanya machukizo makubwa mbele za Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com