“Wakapiga kelele tena, Msulibishe. Pilato akawaambia, Kwani, ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulibishe. Pilato akipenda kuwaridhisha makutano, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulibiwe”, Mk 15:13‭-‬15 SUV.

Kisa hichi cha Yesu kinatufundisha mengi katika maisha yetu, zipo nyakati ngumu watu hujikuta na kukosa njia ya kutokea.

Wakati Pilato amekosa kosa la Yesu, wapo watu walikuwa wanapiga kelele asulubiwe, inaonyesha wazi wananchi walikuwa wana nguvu ya kushawishi jambo zuri au baya na kiongozi akalifuata.

Pilato alikuwa ni kiongozi mkubwa, kutokana na nafasi yake aliweka wazi kuwa haoni kosa la Yesu. Lakini wengi walipiga kelele za kukataa kile alikisema.

Hii tunakutana nayo sana kwenye maisha yetu, wakati mwingine watu wanatushtumu kwa mambo ambayo hatujafanya kabisa.

Walio na makusudi mabaya na sisi wanaweza kutengeneza idadi kubwa ya watu ili kusapoti jambo baya lililokusudiwa kwetu.

Kwa kuwa wengi huamini sauti ya wengi, tutaweza kuingia kwenye hatia kwa jambo ambalo hatukulifanya kabisa.

Zipo hila, mtu anapotengeneza hila kwako, ili akumalize atatafuta wafuasi wanaomsapoti katika kukuona wewe hufai.

Anapofanikiwa kupata kundi linalomsapoti katika hila zake, ujue utafungwa au utaingia kwenye hatia kwenye jambo ambalo hukuhusika kabisa kulifanya.

Tunapaswa kujikabidhi sana kwa Mungu, yapo mambo mabaya yanaweza kutengezwa na wabaya wetu. Na ubaya huo ukapata nguvu kwa kuungwa mkono na idadi kubwa ya watu.

Mtetezi wako awe Mungu, kwa chochote kile kitakapokupata cha kusingiziwa, haijalishi idadi kubwa wanataka uangamie. Mungu atakushindia na ukweli utajulikana.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest