Wapo watu ni wafuatiliaji wazuri sana kwa kile unasema/unafundisha, hawawezi kukosa mafundisho yako ya Neno la Mungu. Wakikosa siku hiyo watahakikisha wamepata CD/DVD zako, kama unafundisha kwa njia ya kuandika makala, watahakikisha wamesoma makala yako.

Hakuna siku watakubali ipite ukiwa unafundisha, siku zote watahakikisha wamepata mafundisho yako uliyofundisha. Unaweza usijue sana kama wanakufutilia ila wanakuwa makini sana kujua leo umefundisha nini, leo umekuja na jipya gani.

Mfano mzuri ni mimi, nina blog ambazo siku haipiti bila kusoma machapisho yake, tena zile blog ninazozipenda nimeweka email yangu. Ili niwe napata taarifa moja kwa moja pale makala ikienda hewani siku hiyo, siku nyingine nakuwa nimetingwa sana ila nitahakikisha nasoma hata kwa siku inayofuata.

Unaweza kuona ni kiasi gani mtu anaweza kuwa mfuatiliji mzuri sana wa maarifa/mafundisho mbalimbali ya watumishi wa Mungu au watu mbalimbali wanaotoa maarifa mazuri ya kimwili. Yanaweza yakawa masomo ya afya, biashara, malezi ya watoto, na nk.

Pamoja na kufuatilia huko, wapo watu watakuwa wasikiaji tu lakini kwenye matendo hakuna kitu. Wapo watu watakuwa wasomaji wako wazuri wa machapisho unayotoa ila wakawa sio watu kuyaweka kwenye matendo yale wanayojifunza.

Ndivyo ilivyo leo hata katika injili, watu watasikia vizuri habari za kuacha dhambi wataonyesha kubadilika, lakini hawatachukua hatua yeyote. Watu watasikia vizuri habari za kuzaliwa mara ya pili ila wataacha hapo yote waliyoyasikiliza/waliyojifunza kwako.

Hebu tuangalie Neno la Mungu linasemaje kuhusu haya ninayokueleza hapa, unaweza kufikiri naeleza habari za kusadikika.

Rejea: Nawe, mwanadamu, wana wa watu wako husimulia habari zako karibu na kuta, na ndani ya milango ya nyumba zao, na kuambiana, kila mtu na ndugu yake, wakisema, Haya! Twende tukasikie ni neno gani hilo litokalo kwa BWANA. Nao huja kwako kama watu wajavyo, nao hukaa mbele yako kama watu wangu, nao husikia maneno yako, wasiyatende; maana kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye upendo mwingi, lakini mioyo yao inatafuta faida yao. Na tazama, wewe umekuwa kwao kama wimbo mzuri sana, wa mtu mwenye sauti ipendezayo, awezaye kupiga kinanda vizuri; maana, wasikia maneno yako, lakini hawayatendi. EZE. 33:30‭-‬32 SUV.

Maneno watayoyasikia kwako wataona kama unawapigia nyimbo nzuri na laini masikioni mwao. Utawaeleza weee lakini kesho utawakuta wapo vile vile na watataka kukusikiliza tena kile unasema.

Utawaambia soma Neno la Mungu, utawaona kama vile ni watu waliokuelewa, kesho utawakuta wapo vile vile walivyokuwa zamani.

Utawaeleza umhimu wa kupenda mafundisho ya Neno la Mungu na kutoa muda wao wa kuhudhuria ibada za kanisani. Wataonyesha kukuelewa vizuri ila wakishaachana na wewe, hutawaona wakifanya yale ulikuwa unasisitiza kuhusu umhimu wa kuhudhuria ibada za kanisani.

Utawaambia acheni kuabudu sanamu, mwabuduni Mungu wa kweli, wataonyesha kama vile wamekuelewa vizuri. Kesho utawakuta wapo na masanamu yao wanayaabudu vizuri sana bila wasiwasi wowote.

Unaweza kufika wakati ukavunjika sana moyo ila fahamu hili, wewe utakuwa umenawa mikono kuhusu wao. Mungu hatakudai damu zao mikononi mwako, maana huna hatia tena juu yao. Hili linapaswa kuwa jambo la faraja kwako unapojikuta unataka kukata tamaa.

Mungu atusaidie sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081