Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, habari za muda huu, Karibu tuendelee kupeana mambo ya kujenga katika maisha yetu.
Tunajifunza hata katika maandiko Matakatifu, kila unalofanya jema kwa wengine, linabaki kuwa alama nzuri ndani ya mioyo ya watu.
Wema wako uliofanya leo, unaweza kuwa faida kwa watoto wako hata kama hutokuwepo duniani. Kila uliyemtendea mema akawa na moyo wa shukrani ndani yake, anaweza kujitoa kwa familia yako kuisaidia, kwa ajili tu ya wema wako uliomfanyia siku za nyuma.
Elewa pia, sio kila wema ulioutenda unaweza kuwa faida kwako, wema mwingine unaweza kugeuka fimbo kwako. Ndio maana unapaswa kujua kwamba, unapotenda mema usiweke mategemeo ya kurudishiwa mema.
Wengi wetu tumejikuta tunapotea njia kwa kuwatendea wengine mema, alafu wao wakaturudishia mabaya kwa njia ambayo hatukutegemea.
Tunaweza kurudisha fadhila kwa waliotutendea mema, wakatokea wengine wakaona tunafanya vile kwa sababu tunataka kitu fulani kwao.
Hofu yao ya kunyang’anywa vitu vyao, inaweza kupelekea tukaingizwa kwenye matatizo ambayo hukutegemea kabisa kukutana nayo.
Labda hujanielewa vizuri ninachosema hapa; nasema hivi, sio kila shukrani utakayoirudisha/utakayoitoa kwa waliokutendea mema. Itaweza kueleweka moja kwa moja kwa wengine, kuwa ulichofanya ni kwa ajili ya kurudisha fadhila zako tu.
Unaweza kunielewa zaidi kwa kusoma maandiko haya Matakatifu;
Naye Daudi akasema, Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahashi, kwa kuwa babaye alinitendea mimi wema. Basi Daudi akapeleka wajumbe ili kumtuliza kwa habari za babaye. Wakaja watumishi wa Daudi katika nchi ya wana wa Amoni kwa Hanuni, ili wamtulize.
Lakini wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia Hanuni, Je! Waona Daudi amheshimu babayo kwa kukupelekea wafariji? Je! Hawakukujia watumishi wake ili kuiangalia nchi, na kuiangamiza, na kuipeleleza?
Basi Hanuni akawatwaa watumishi wa Daudi, akawanyoa, akawakatia nguo zao katikati, hata matakoni, akawatoa waende zao. 1 Nya 19:2_4.
Umeona hapo kilichowatokea watumishi wa Daudi, badala Hanuni kuona Daudi ameleta watumishi wake kwa ajili kumfariji yeye. Hanuni akajazwa maneno mabaya na watu wengine mpaka kumpelekea kuwafanyia watumishi wa Daudi vitendo vibaya.
Huenda haya yamekutokea katika maisha yako, labda ulifanya jambo kwa ajili ya kujitoa kwa ajili ya mtu fulani. Badala ya kueleweka vyema ukajikuta unaeleweka vibaya na unaingia katika matatizo.
Hawa watumishi wa Daudi, safari yao iligeuka majuto maana hawakuruhusiwa tena kukaa na mfalme wao aliyewatuma, bali waliambiwa wakakae Yeriko mpaka waote ndevu zao.
Rejea; Wakaenda watu wakamwambia Daudi jinsi walivyotendewa wale watu. Naye akatuma watu kuwalaki; kwa sababu watu hao walikuwa wametahayarika sana. Mfalme akasema, Ngojeni Yeriko, hata mtakapoota ndevu zenu, ndipo mrudi. 1 Nya 19 :5.
Umeona hapo wema unavyoweza kugeuka majuto/huzuni kwako, pamoja na kugeuka huzuni kwako, usije ukaacha kutenda mema. Kutenda wema ni akiba yako duniani na mbinguni.
Mungu akusaidie kuelewa haya usije ukaacha kutenda mema kwa kuumizwa vibaya, hufanyi kwa sababu ya watu wakuone, unafanya kwa sababu moyoni mwako unalijua NENO la MUNGU.
Bila shaka kuna kitu umeondoka nacho cha kukusaidia katika maisha yako, kifanyie kazi ulichojifunza ili kiwe msaada kwako.
Nakutakia wakati mwema.
Samson Ernest.
+255759808081.