Kabla ya kuijua thamani yako mbele za Mungu, unaweza kunyanyaswa sana na vitu vingi katika maisha yako ya kila siku.

Kutokujua kwako au kutokuwa na maarifa sahihi ya Neno la Mungu, unaweza kujikuta unyanyaswa hata na paka(nyau) akilia nje. Na unaweza kupata hofu nyingi pale unaposikia paka anatembea juu ya paa la nyumba yako.

Tofauti kabisa na mtu aliyeokoka sawasawa, alafu akawa anajua yeye ni nani mbele za Mungu. Huyu mtu ujasiri wake na huyu ndugu mwingine asiyejua yeye ni nani mbele za Mungu, hawa ndugu wakikaa pamoja. Hata mitazamo yao, namna ya kufikiri kwao kupo tofauti kabisa.

Unapaswa kuelewa au tunapaswa kuelewa kwamba, tukishakubali kuokoka, Yesu Kristo akawa Bwana na mwokozi wa maisha yetu. Tunapaswa kuelewa sisi ni mboni ya jicho la Mungu wetu aliye hai.

Yeyote atakakugusa kwa nia yeyote ile iwe mbaya au iwe nzuri, uwe na uhakika amegusa mboni ya jicho la Mungu wako. Ndio uwe na uhakika mtu huyo amegusa mboni ya jicho la Bwana Mungu wako.

Unaweza usiwe na uhakika, unaweza ukawa una mashaka na haya ninayokueleza hapa ila unapaswa kufahamu hivyo. Ukishafahamu hivyo utaanza kujiona ni mtu wa tofauti kabisa, tena utamchukulia au hutomzama Mungu kama zamani.

Neno la Mungu linatuthibitishia haya, na linatupa ujasiri wa kujiona ni watu tuliochaguliwa na Mungu mwenyewe. Ni jinsi gani hatupaswi kuwa na mashaka juu ya maisha yetu.

Rejea: Kwa maana BWANA wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake. ZEK. 2:8 SUV.

Haleluya, habari njema kwako ni kwamba, yeyote atakayekugusa wewe katika maisha yako, uwe na uhakika ameigusa mboni ya jicho la Mungu wako. Tena huna haja ya kupambana na huyo mtu/watu, maana wanapambana na aliyekuita, wanapambana na aliyekuchagua, na wanapambana na aliyekuokoa katika maisha ya dhambi.

Kama wewe ni mboni ya jicho la Mungu, una mashaka gani juu ya wachawi, unaogopa nini haswa katika maisha yako na wakati yupo ambaye anakutetea maisha yako. Na halali usiku na mchana, anakuchunga wewe.

Udhaifu wako wa kimwili, hali uliyonayo, isikufanye ukajiona wewe si kitu mbele za Mungu. Hakikisha unatembea kifua mbele ukiwa na uhakika wewe ni mtu wa namna fulani ya juu sana mbele za Mungu.

Mimi ni mboni ya jicho la Mungu, wewe ni mboni ya jicho la Mungu. Linda sana utakatifu wako usije ukaruhusu dhambi iingie kwako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.