
Hili najua umewahi kuliona hata shuleni, kuna mwanafunzi mlikuwa mnadharau kutokana na kushindwa kwake kwenye masomo au kutokana na hali yake ngumu kimaisha.
Mkaenda naye hivyo hivyo hadi mnamaliza shule, na huenda matokeo yake hayakuwa mazuri sana kama ya wengine, baadaye mlipotezana kila mtu akaenda zake.
Baadaye sana baada ya miaka mingi kupita mlikutana na huyo huyo mtu mliyekuwa mnamwona ni mtu asiyeweza kufika mahali popote kutokana na alivyokuwa.
Unashangaa ofisi uliyeingia unamkuta yeye ndiyo boss wa ofisi hiyo, aliwezaje kufika hapo, hiyo ni habari nyingine kabisa ila wakati huo yeye ni boss. Na ukute wewe ndiye uliyeenda kuomba kazi mahali hapo au uliomba ukapata hapo ulikuwa unaenda kuripoti kazini ila hukujua kama mwenye ofisi ndio huyo.
Mfano huo wa shule unaweza usiulewe vizuri kutokana labda umemaliza shule siku nyingi, labda tuseme una mtoto wako, mtoto ambaye ulikuwa unamwona ni mtu wa kushindwa tu hadi ukafika mahali ukawa unamnenea vibaya.
Mtoto ambaye hukuwa ukimpa sana kipaumbele kutokana na uzito wake wa kupokea kile unamwelekeza, ila kupitia mtoto yule yule uliyemdharau ndiye amekuja kuwa mtoto mwenye mafanikio makubwa na msaada kwenu wazazi.
Ipo mifano mingi sana, ndio maana huwa nasema usimdharau mtu unayemjua na usiyemjua, hata yule unayedhania unamjua hujui Mungu anamuwazia nini juu ya kesho yake.
Mungu alivyo huwezi kujua fulani atakuwaje kesho, wapo watu walidharauliwa sana walivyoanza huduma zao ila leo ni watumishi wakubwa wanaomtumikia Mungu kwa viwango vikubwa sana.
Lakini ukisikiliza shuhuda zao ndio unajua Mungu amewatoa mbali mno, unaweza ukawa hujapata nafasi ya kusikia hilo ila tunao watumishi wengi kwenye Biblia ambao walikuwa ni watu wanaoonekana wa kawaida sana.
Tunaona mwisho wake walikuja kuwa watumishi wakubwa, mfano mzuri ni Daudi, Daudi alikuwa ni mchunga kondoo za baba yake. Hakuna mtu alikuwa anajua huyo ni mfalme ajaye, wazazi wake wangejua ni mfalme ajaye huenda wasingekubali akachunge kondoo huko porini.
Hata wakati baba yake Daudi anajiwa na Samweli nyumbani, kwa ajili ya kumpaka mafuta yule aliyechaguliwa na Mungu kuwa mfalme baada ya Sauli kumkosea Mungu. Yese hakujua kama mtoto wake huyo ndiye aliyekusudiwa na Mungu.
Hapa tunajifunza nini? Vile vinyonge watu wasivyovidhania ndivyo Mungu huviinua ili vile ambavyo watu wanaviona ni maana sana viweze kuonekana si kitu.
Rejea: Bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko. 1 KOR. 1:27-28 SUV.
Usimdharau mtu, wala usijidharau kwa namna yeyote ile, hata kama kwa sasa unaonekana umechoka sana kimaisha, kama ni mwaminifu mbele za Mungu na unajituma kwa hayo mambo madogo uliyonayo sasa. Itafika wakati ambao utashangaa unakuwa juu zaidi ya ulivyo sasa.
Cha msingi ni kuwa mwaminifu mbele za Mungu na kuendelea kujitoa kwa moyo wako wote, kile ambacho unapata nafasi kukifanya unakifanya kwa bidii zako zote. Mungu lazima akuinue tu, maana maandiko yanasema hakuna mwenye haki aliyewahi kuachwa na Mungu.
Simama na Mungu wako, lea watoto wako vizuri, hata kama baba yao amekukimbia na kukuachia watoto wote. Jibidiishe kuwalea katika maadili mema huku ukiwaombea kwa Mungu, maana hujui unalea viongozi gani wa kesho, wala hujui unalea wahubiri gani wa kesho.
Pamoja na unyoge wenu, Mungu huwa haangalii kama mwanadamu atazamavyo/aangaliavyo saa ikifika uliyekuwa unaonekana si kitu, Mungu atakufanya uonekane ni mtu mbele za watu.
Usijipuuze na kujiona hufai, wewe ni wa thamani mno mbele za Mungu, endelea kusimama na Yesu Kristo, endelea kutunza utakatifu wako, ishi maisha ya kumpendeza Mungu. Saa yako yaja utacheka kicheko kikuu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com