“Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe”, 1 Kor 6:18 SUV.
Zipo dhambi nyingi zilizo chukizo mbele za Mungu, lakini hizi dhambi zinatofautiana katika utendaji wake na viwango vyake.
Zinaa ina utofauti na dhambi zingine, hili ni tendo ambalo humchukiza sana Mungu kwa namna ya pekee ukilinganisha na dhambi zingine.
Tendo hili huligusa moja kwa moja na kulinajisi hekalu la Roho Mtakatifu, ambalo Mungu ameagiza tusiliharibu.
Mtume Paulo anatuonya kuhusu hili la zinaa, watu wanapaswa kuikimbia kabisa zinaa bila kujali mazingira na hali zao.
Yusufu ni mfano mzuri wa hili, hakuangalia itakuwaje, hakuogopa nafasi yake itakuwaje, alimkimbia mke wa Potifa kwa kile kitendo alicho dhamiria kukifanya kwake.
“Huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje”, Mwa 39:12 SUV.
Tunaweza kusema bora kukubali kufanya zinaa ili usiharibu nafasi yako ya kazi, Yusufu atakuambia yeye hakujali hilo, alimkimbia mke wa Boss wake.
Zinaa haichekewi, ukicheka nayo itakuharibia maisha yako ya kiroho na kimwili, inaua haraka uhusiano wako mzuri na Mungu, na inaua ndoa yako nzuri.
Utachagua ulinde kibarua chako kwa kufanya uasherati au uzinzi na mwajiri wako? Ama utaamua kulinda uhusiano wako mzuri na Mungu.
Utachagua kupatiwa msaada wa kifedha kwa kuzini na mwanaume/mwanamke? Au utakubali ufe na shida yako ila usiharibu uhusiano wako na Mungu.
Utachagua upate nafasi ya kazi kwa kufanya uasherati/uzinzi na anayetoa nafasi hiyo? Au utakubali ukose hiyo kazi kulinda uhusiano wako mzuri na Mungu wako.
Mambo haya yapo mikononi mwako, uchaguzi upo mikononi mwako, usuke au unyoe, haya yapo ndani ya uwezo wako, uhitaji kwenda kuomba ushauri kwa mtu mwingine.
Ujue hakuna sababu yeyote ya kukufanya ujiingize kwenye zinaa, haijalishi una shida kiasi gani, hupaswi kukubali kufanya tendo hili baya mbele za Mungu.
Watu waliopuuza hili wanajutia maisha yao, gharama ya zinaa ni kubwa kuliko shida aliyokuwa nayo mtu, zinaa inagusa kiroho na kimwili.
Acha kujifariji dhambi zote ni sawa, elewa maumivu ya kuchomwa moto hayafanani na kuchomwa mwiba au mbigiri au sindano.
Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081