
Ili uonekane mwenye haki mbele za Mungu, hiyo haki haitokani na matendo ya sheria, bali inatokana na imani yako mbele za Mungu. Sheria hazitufanyi tuhesabiwe haki, bali mwenye haki ataishi kwa imani.
Tunaweza kuhangaika sana kushika sheria zilizoamriwa, tukifikiri tunaweza kuzishika ipasavyo hizo sheria na tukampendeza Mungu wetu. Tutakuwa tunajidanganya sana, maana hakuna anayeweza kushika sheria zote alafu akampendeza Mungu.
Kuishi kwetu kama wakristo wenye safari ya kwenda mbinguni tunapaswa kuishi kwa imani, na si kwa matendo ya sheria, imani yetu iliyothabiti mbele za Mungu, inatufanya tuhesabiwe haki.
Rejea: Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. GAL. 3:11 SUV.
Ikiwa baba yetu wa imani ni Ibrahim, tunapaswa kuishi kwa imani, na si kwa matendo ya sheria, tukiishi kwa imani tutahesabiwa haki mbele za Mungu. Na sio matendo ya sheria ndiyo yatatufanya tuhesabiwe haki.
Biblia inasema amelaaniwa mtu yule ambaye hayafanyi yote yaliyoamriwa na sheria, hii inaonyesha ni jinsi gani ilivyo ngumu kuishika sheria yote na ukampendeza Mungu wako. Ndio maana Mungu kupitia mwanaye wa pekee, akaja kutukomboa katika laana.
Rejea: Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. GAL. 3:10 SUV.
Ndugu usije ukajidanganya, kuishika sheria yote iliyoandikwa katika kitabu cha torati ni ngumu sana, na ukisema utashika nusu na mengine unaacha. Maana yake upo chini ya laana, maana yule asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, mtu huyo amelaaniwa.
Ipi bora? Kuwa chini ya sheria, au kuwa katika neema ya Kristo, maana tumeona hapa kuishi katika sheria zote tukazifuata kama inavyotakiwa kuishi, haiwezekani kabisa.
Fahamu kuanzia sasa, kuhesabiwa kwetu haki mbele za Mungu, hatuhesabiwi kwa matendo ya sheria, kwa sababu mwenye haki ataishi kwa imani. Kama ataishi kwa imani, sheria haina nafasi kwa mtu aliyemwamini Kristo, maana kuhesabiwa kwake haki si kwa matendo ya sheria.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.