Mungu anapotutuma tukaifanye kazi yake mara nyingi huwa tunajidharau na kujiona hatuwezi kufanya, kinachotufanya tujione hivyo ni kujitazama kimwili.

Mazingira tuliyozaliwa yanaweza yakawa na mchango mkubwa sana katika maisha ya mtu, Mungu anakuwa amemwamini kufanya kazi yake ila yeye anakuwa hajiamini kabisa.

Ukimgusa anaanza kukuambia mimi siwezi, sababu haswa ya kusema hivyo ni vile anavyojitazama kwa nje, anasahau pamoja na hali aliyonayo Mungu ameona anafaa.

Sio vizuri kujidharau, maana kujidharau hupelekea uone kila jambo kubwa unaloambiwa ufanye, utajiona huwezi, usije ukafikiri ni heshima kwako kujiona huwezi. Wala hutoonekana mnyenyekevu sana kwa kusema huwezi kufanya jambo uliloagizwa.

Rejea: Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? KUT. 3:11 SUV.

Wenye kauli kama ya Musa ni wengi, wanaoweza kujiona hawawezi ila cha msingi ni kumsikiliza Roho Mtakatifu anavyokuelekeza ufanye. Hutaeleweka sana ila aliyekutuma atakuwa pamoja na wewe.

Ikiwa Mungu amekuchagua kwenye eneo/nafasi fulani umtumikie, uwe na uhakika amekuamini, bila kujalisha wangapi wanakuona hutoweza. Jua jambo moja tu, Mungu amekuamini unaweza.

Rejea: Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu. KUT. 3:12 SUV.

Neno hili la Mungu linatupa nguvu ya kufanya kile tunachoagizwa/tunachotumwa, unaweza ukawa hukuwahi kusimama uhubiri habari za Yesu. Pamoja na hilo unaweza ukaambiwa kuanzia sasa utakuwa mhubiri wa injili.

Unapoambiwa hivyo usikatae, msikilize Mungu anavyokuelekeza ufanye, maana yeye ameahidi atakuwa pamoja nawe. Hutofanya huduma aliyokupa peke yako, atakuwa nawe hatua kwa hatua.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081