“Na watu wote walikuwa wakilia na kumwombolezea; akasema, Msilie, hakufa huyu, bali amelala usingizi tu. Wakamcheka sana, maana walijua ya kuwa amekwisha kufa”, Lk 8:52‭-‬53 SUV.

Wakati mwingine huwa tunaonekana kama tumechanganyikiwa au hatuna akili sawa sawa, hasa tulioamini.

Kuna mambo unaweza kumweleza mtu au kuna maono unaweza kumshirikisha mtu akaishia kukucheka au kukudharau.

Usipokaa vizuri unaweza kuvunjwa moyo, ukaishia kuacha kile Mungu amekupa ukifanye katika maisha yako ya huduma. Haijalishi ulikuwa na huduma nzuri sana.

Jambo hili alikutana nalo Yesu, wakati anawaeleza huyu mnayesema amekufa “hakufa bali amelala usingizi”, waliishia kucheka sana.

Ukiwa mfuasi wa Kristo, yapo mambo hutoeleweka hata kwa mzazi wako, zaidi utaishia kuchekwa na kuambiwa maneno ya kejeli kukatisha tamaa.

Yesu hakujali kucheka kwao, wala hakuanza kupambana nao kwa ile dharau waliyoonyesha kwake. Yeye alienda moja kwa moja kwenye lengo, na mwisho wakaishia kushangaa muujiza uliotokea.

“Akamshika mkono, akapaza sauti, akisema Kijana, inuka. Roho yake ikamrejea, naye mara hiyo akasimama. Akaamuru apewe chakula”, Lk 8:54‭-‬55 SUV.

Dunia ya sasa imejaa wajuaji wengi, hata asiye na uhakika na anachoamini au anachoongea, ataongea kwa ujasiri utafikiri ni cha kweli.

Tunapaswa kuangalia neno la Mungu linasema nini juu yetu, yapo mambo ni makubwa na mazito. Mambo ambayo hatuwezi kueleweka haraka ila tusiogope, tuendelee kumwamini Mungu.

Punguza kujipambania mwenyewe, Yesu aliyekuita atakupambania, wewe uwe mnyenyekevu mbele za Mungu. Acha makeke yasiyo na sababu, wito na huduma uliyonayo Mungu amekupa.

Kikubwa usiende kinyume na neno la Mungu, ukiwa huendi kinyume hata kama watu wanakucheka na kuonyesha dharau, simamia kile Mungu amekupa.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081