Haleluya,

Ipo siku unaweza kuja kujutia jinsi ulivyotumia akili zako kidogo kumzalia Bwana matunda yaliyo mema. Jinsi ulivyotumia akili zako kidogo kufanya huduma aliyokupa Mungu ndani yako.

Wapo watu wavivu kiasi kwamba hata kutenga muda kufikiri ili kupata suluhisho kwa jambo dogo linalomsumbua, inakuwa ngumu kwake au anaona mateso kwake. Anachofanya ni kuachana nalo.

Yapo mambo mengi sana tunayafanya bila kutumia akili ipasavyo, badala yake tumeendelea kupata matokeo yale yale ya kila siku.

Unakuta mtu anafanya kazi zake ofisini utafikiri amelazimishwa kukaa pale, hana anacholeta ofisini wala hakuna mabadiliko yeyote yanayosababishwa na yeye. Yeye anachoangalia mwisho wa mwezi aingiziwe mshahara wake bank basi.

Lakini kukaa chini kufanya kazi kwa kiwango cha kutumia akili aliyonayo, anaona tabu kwake. Changamoto ndogo inakuwa kubwa kutokana na kushindwa kutumia akili alizonazo.

Mungu ameweka hazina kubwa mno ndani yetu, hili nimelishuhudia mwenyewe, sikujua mapema ila sio sababu ya mimi kushindwa kufanya mambo mazuri ya kumtukuza Mungu.

Hata katika huduma zetu, mara nyingi sana tumetumia uwezo mdogo wa akili kufanya huduma. Wakati Mungu ametupa akili ili tuweze kuzitumia katika huduma zetu alizotupa Mungu, lakini sisi tunaona haina haja kuzitumia akili zetu.

Nafikiri watu huwa wanachanganya pale Mungu anaposema tusizitengemee tu akili zetu. Ni kweli kabisa tunapaswa kumtanguliza Mungu kwa kila hatua ya Maisha yetu. Ila sio kwamba tusitumie akili zetu kufanya mambo mengine makubwa zaidi.

Kushindwa kwetu kutumia akili alizotupa Mungu, tumejikuta tupo vile vile miaka nenda rudi. Wakati tulipaswa kuwa hatua fulani kimaendeleo kwa kadri tunavyozidi kukua kimwili na kiroho.

Rejea: Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? ZAB. 94:8 SUV.

Hebu jiulize lini huwa unakaa ukaumiza kichwa utawazaje kuboresha kile unafanya. Lini umekaa ukaumiza kichwa ukiwaza kutengeneza kitu ambacho hakijawahi kuwepo ila ni muhimu sana kiwepo kwa dunia ya sasa.

Akili zako unazifanyia nini au umeziacha tu, au hujui chochote kuhusu kutuu akili zako. Mtunga Zaburi anasema lini utapata akili ya kufanya mambo ya kiMungu yakaenda vizuri. Ni wewe kutafakari na kuchukua hatua stahiki kujiokoa na uzembe uliokuwa nao.

Hakikisha unatumia akili kwenye familia yako, hakikisha unatumia akili kwa mke/mume wako, uwe na uwezo wa kumtambua mwenzako anahitaji nini. Sio unaishi unafikiri Mungu hajakuwekea kipengele cha akili, wakati unacho ila umekikalia bila kukitumia.

Hakikisha unatumia akili ipasavyo kwenye biashara yako, sio miaka yote upo vile vile; wala hakuna mabadiliko yeyote yale kwenye kile unachofanya. Wenzako ulioanza nao, leo hawafanyi tena kama mlivyoanza, ila wewe umeng’ang’ana na mfumo ule ule wa zamani.

Hakikisha ulipoajiriwa unatumia akili zako ipasavyo, fanya kazi zaidi ya matarajio, jiongeze zaidi kwa kutumia akili zako. Usifanye kama umelazimishwa kuwepo ofisi ile, usifanye kama upo pale kwa bahati mbaya. Hata kama kwa bahati mbaya ifanye kuwa haikosewa wewe kuwepo hapo.

Rejea:
Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka. Mithali 10:8 SUV

Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu. Mithali 10:14 SUV

Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake; Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa. Mithali 12:8 SUV

Fanya vitu vya kiwango kwa kutumia akili ulizopewa na Mungu, tumia akili zako ipasavyo kujiepusha na mitengo ya ibilisi shetani. Akili zako zimepakwa mafuta ya Roho Mtakatifu, hakikisha unayatumia hayo mafuta kumzalia Mungu matunda mengi na mazuri.

Eneo lolote lile ulipo, hakikisha unatumia akili zako kuwa suluhisho la wengine kuhusu changamoto mbalimbali wanazopitia. Kwa kutumia akili uliyopewa na Mungu wako, akili zinaweza kumfanya mtu akafanya jambo baya na akili zinaweza kumfanya mtu akafanya jambo zuri.

Omba Mungu afungue ufahamu wako ili uweze kujua umhimu wa kutumia akili zako, maana unaweza kuchukulia kawaida alafu ukakosa vitu vya msingi.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
chapeo@chapeotz.com
www.chapeotz.com
+255759808081.