Upendo kati ya mume na mke, huwezi kuondolewa/kutenganishwa kirahisi na wazazi, ndugu, au marafiki, kwa mwanaume/mwanamke anayejitambua.

Tunaweza kufikiri mzazi au ndugu anaweza kuwa na nafasi kubwa ya kufanya kile anafikiri kwenye ndoa ya mtoto wao. Lakini hili haliwezi kupewa asilimia zote ikiwa wanandoa wale wanapendana.

Ukiwa kama mzazi, au kaka, au dada, au ndugu yeyote yule. Unaweza kumweleza mtoto wako, au dada yako, kaka yako, jambo la siri ya kutaka kumtendea vibaya mume/mke wake.

Ukiwa na uhakika mwingi wa kufanikisha zoezi lako, ukifikiri huyo mke/mume wake ambaye ni mtoto wako, au dada yako, au kaka yako, au ndugu yako.

Ukaona ni rahisi sana, ukweli ni kwamba, ikiwa hao wanandoa wanapendana. Huwezi kuwa na nafasi kwenye ndoa ile kufanya jambo baya unavyotaka wewe kwa mmoja wao.

Hili tunalithibitisha kwa Mikali mke wake na Daudi, ambaye ni mtoto wa Mfalme Sauli wa kumzaa.

Sauli alikusudia kumuua Daudi na mke wake Mikali akazipata habari hizo. Hakukaa kimya kwa sababu baba yake mzazi alikuwa anafanya hilo jambo.

Alisimama na mume wake, akamweleza ukweli, kile ambacho kilikusudiwa na baba yake. Tena kwa uwazi pasipo kificho.

Rejea: Kisha Sauli akatuma wajumbe mpaka nyumbani kwa Daudi, ili wamvizie na kumwua asubuhi; naye Mikali, mkewe Daudi, akamwambia, akasema, Wewe usipojiponya nafsi yako usiku huu, kesho utauawa. 1 SAM. 19:11 SUV.

Upendo wa kweli usio na unafiki ndani yake unaweza kumwokoa mtu.

Bila kujali uhusiano wa mzazi, kama tulivyoona kwa Mikali mke wake na Daudi.

Alioonyesha upendo, utu, uthamani, umhimu mkubwa wa mume wake katika maisha yake.

Hakuishia kumpa ujumbe wa tahadhari, alijitoa kumwondoa nyumbani kwake.

Hakuishia tu kumtorosha, alichukua hatua nyingine ya kuchukua kinyago na kukilaza kitandani kwake kuonyesha uwepo wa mume wake Daudi.

Rejea: Basi Mikali akamtelemsha Daudi dirishani; naye akaenda akakimbia na kuokoka. Ndipo Mikali akakitwaa kinyago, na kukilaza kitandani, akatia na mto wa singa za mbuzi kichwani pake, na kukifunika kwa nguo. 1 SAM. 19:12‭-‬13 SUV.

Unaona hiyo kazi ya Mikali, hii inaonyesha ni jinsi gani alimpenda mume wake. Hakutamani kuona akiuwawa, alifanya kila linalowezekana kumwokoa.

Hapa tunajifunza kitu kingine cha pekee sana, inaonyesha vile upendo unaweza kuleta ujasiri kwa mtu.

Ujasiri wa kumsaidia kufanya jambo kubwa kwa muda mfupi bila kuonyesha hofu, bila kuangalia madhara gani yanaweza kumpata baada ya kutekeleza mpango wake.

Mikali mke wake na Daudi amebeba ujumbe mkubwa sana, ujumbe ambao unafundisha vile upendo wa kiMungu huwezi kukubali mume/mke wako kufanyiwa jambo baya na ndugu zako.

Ingekuwa mwanamke mwingine angekubali kwa sababu baba yake ndiye alikuwa anafanya hilo jambo baya la kuondoa uhai wa Daudi.

Tunaona lawama zilikuja baadaye kwa Mikali, baba yake Sauli alimweleza moja kwa moja. Na Mikali alimjibu baba yake bila kutetereka.

Rejea: Sauli akamwambia Mikali, Mbona wewe umenidanganya hivi, na kumwacha adui yangu aende, hata ameniponyoka? Naye Mikali akamjibu Sauli, Yeye aliniambia, Niache niende zangu; kwa nini nikuue? 1 SAM. 19:17 SUV.

Hili ni somo kwa wanandoa wote, wanapaswa kujifunza somo hili kutoka kwa Mikali. Maana alisimama na mume wake bila kujalisha kitamtokea nini.

Sio wanandoa tu, hata wale wote wanaoona kuna jambo baya limekusudiwa dhidi ya mtu fulani wa muhimu kwao.

Hawapaswi kunyamaza kimya, wanapaswa kuchukua hatua za haraka kumwokoa na hatari iliyo mbele yake.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81