Kama yupo mtu mwenye uwezo wa kumshusha chini mtu, na mwenye uwezo wa kumwinua juu mtu.

Kwa vyovyote vile mtu huyo anaweza akawa anaogopwa na kuheshimiwa sana na watu.

Watu wakishajua hilo, ila kama bado hawajajua hilo wanaweza wakawa wanamchukulia kawaida sana.

Leo unapaswa kuelewa hili, yupo anayeweza kukupandisha juu, na anayeweza kukushusha chini.

Hii ni habari njema kwa upande mmoja, na upande mwingine wa pili inaweza ikawa ni habari mbaya.

Kwanini iwe habari njema na mbaya, kama unaishi maisha matakatifu ya kumpendeza Bwana. Na unaenda vile Mungu anataka, uwe na uhakika kuinuliwa kwako kupo.

Na ikiwa unaenda kinyume na vile Mungu anataka, uwe na uhakika utashushwa chini. Haijalishi ulipiga hatua kubwa kiasi gani katika maisha yako.

Rejea: BWANA hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. 1 SAM. 2:7 SUV.

Hili linapaswa kuwa fundisho lako kuu miongoni mwa mafundisho unayopaswa kuwa nayo katika maisha yako.

Siku zote unapaswa kuelewa mwenye uwezo wa kumshusha mtu ni Mungu, na mwenye uwezo wa kumpandisha mtu viwango vya juu ni Mungu mwenyewe.

Hapa unapaswa kuwa makini sana, maana unaweza ukafika mahali ukawa juu. Ukawa unajulikana huku na kule, umaarufu wako ukawa mkubwa kihuduma, au kibiashara, au kikazi.

Usipokuwa na muda wa kutosha na aliyekupa huo umaarufu, ni rahisi sana kiburi kukuingia na kujiona wewe ni wewe. Hakuna mwingine kama wewe mwenye uwezo mkubwa.

Watu wasilojua ni kwamba hata yule ambaye alikuwa anaonekana si kitu mbele za watu. Kutokana na hali yake ya maisha ilivyo, Mungu anaweza kufanya jambo ambalo macho hayataamini.

Rejea: Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina BWANA, Naye ameuweka ulimwengu juu yake. 1 SAM. 2:8 SUV.

Kupitia neno hili inatupasa tuwe na subira/uvumilivu, kuusubiri wakati wa Bwana ni heri sana kuliko jambo lolote lile.

Haijalishi upo mazingira fulani magumu sana na huoni dalili ya kutoka hapo ulipo. Uwe na uhakika wakati wa Bwana ukifika atakutoa hapo ulipo na kukuketisha na wakuu.

Muhimu ni kuendelea kumtumainia Bwana Yesu siku zote, na kuhakikisha neno la Mungu linakuwa kwa wingi ndani yako.

Ikiwa kwenye huduma, kazi, biashara, Yesu atakupandisha viwango vya juu zaidi ukimtumainia yeye siku zote za maisha yako.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81