
Ahadi ya Yesu Kristo kwetu sisi wanafunzi wake ni tubatizwe kwa maji, na kwa Roho Mtakatifu, baada ya ubatizo wa maji hatua inayofuata unapaswa kubatizwa kwa Roho Mtakatifu.
Wengi wetu tumefanikiwa kubatizwa na ubatizo mmoja tu wa maji, ila ubatizo wa Roho Mtakatifu bado hatujabatizwa nao. Ambapo ni jambo la muhimu sana kwa kila mkristo kuwa nacho.
Ile subira na kiu ya kutamani kujazwa na Roho Mtakatifu, wengi hawana kabisa hiyo kiu siku hizi, ndio maana mtu akishabatizwa na maji anaona inatosha kubatizwa.
Ubatizo wa pili ambao ni ubatizo wa Roho Mtakatifu ni ubatizo wa muhimu sana kwa mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni, kuokoka ni hatua nyingine, na kubatizwa kwa maji ni hatua nyingine, na kujazwa Roho Mtakatifu ni hatua nyingine pia.
Kiu kubwa ambayo mtu yeyote aliyeokoka anapaswa kuizingatia, ni kuhakikisha hatua hizi mbili anazipatia. Hasa kujazwa Roho Mtakatifu baada ya kubatizwa na maji, ni jambo la msingi sana kwa kila mwamini.
Usiseme nimeokoka imetosha, Usiseme nimebatizwa kwa maji inatosha, bado haijatosha, unapaswa kubatizwa kwa Roho Mtakatifu.
Rejea: Ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. MDO 1:5 SUV.
Mchungaji wako akibatiza kwa maji, hakikisha unapatizwa na kwa Roho Mtakatifu, jawa na nguvu za Roho Mtakatifu. Sio jambo la kujihoji sana, hii ni ahadi ambayo kila mmoja anapaswa kuipokea.
Usibakie na ubatizo wa mchungaji wako ambao tunauita ubatizo wa Yohana, chukua hatua ya pili ya kubatizwa na ubatizo wa Roho Mtakatifu, utakuwa mtu imara na aliyejaa ujasiri mwingi wa kiMungu.
Batizo zote ni muhimu, wa maji, na wa Roho Mtakatifu, usipuuze ubatizo wa aina yeyote kati ya hiyo, hakikisha unatimiza haki yote. Na sio kitu kigumu kwako kufanya, ukiwa na kiu ya Roho Mtakatifu utaweza kumpokea.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com