Mahali ambapo mtu anapitia unaweza usielewe sana kutokana na huwezi kujua kinachomsibu kwenye moyo wake ni nini.
Yapo mambo mengi sana ambayo yanaweza kumkosesha mtu amani ya moyo wake, akakosa amani kabisa ya kuishi kwake.
Na mtu anapokosa amani ndani ya moyo wake, mtu huyo hawezi kufurahia maisha yake, wokovu wake, huduma yake, kazi yake, ndoa yake na mengine yanayofanana na hayo.
Amani inaweza ikatoweka kwa mtu kutokana na hali fulani ya maisha anayopitia kwake, hii inaweza ikamfanya akose amani.
Mtu mwingine anaweza akakosa amani kutokana na kutofanikiwa jambo lake alilomwomba Mungu amfanikishe.
Mwingine anaweza akakosa amani kutokana na kutokuwa na uhakika wa kesho yake, mazingira ya nje yanakuwa yanawatia hofu kubwa na kukosa amani.
Haijalishi unapitia shida gani katika maisha yako, wala haijalishi hukumbuki Mara ya mwisho kuwa na amani ndani ya moyo wako ilikuwa lini.
Leo Mungu akupe amani ya moyo wako, haijalishi ni jambo gani linakukabili na kukufanya ukose amani ya moyo wako. Bwana akupe amani ya moyo wako.
Rejea: BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani. HES. 6:26 SUV.
Haijalishi ni mzigo gani ulionao kwenye maisha yako, mwamini Mungu atakupa amani ya moyo wako. Katikati ya jangwa utamwona Bwana akikupa amani ya moyo wako.
Usije ukaangalia uzito wa jambo linalokukabili na ukaona haiwezekani Mungu akakupa amani yake. Ukiona haiwezekani ujue haitawezekana kweli, ila ukiona na ukiamini inawezekana itawezekana kweli.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com