Kupita kwenye hali za kuchoka na kuzimia mioyo yetu, tunapita sana, tena wakati mwingine tunaona kama giza mbele yetu.

Nyakati kama hizo ambazo zinatufanya tuwe wanyonge, ambazo wakati mwingine huwa tunaona mambo hayaendi vile tulitarajia.

Hutufanya tuugue na wakati mwingine kuvunjika mioyo yetu, tunapofika kipindi cha kuvunjika moyo na kuona ugumu mbele yetu. Neno la Mungu linatutia moyo kwa namna ya pekee mno.

Rejea: Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia. ISA. 40:29‭-‬31 SUV.

Sijui unaona faida kiasi gani kujenga imani yako kwa Mungu aliye hai, sijui umeweka nguvu kiasi gani ya kumtegemea Mungu.

Nimesikia uhai wa Kristo ndani yangu baada ya kusoma mistari hiyo, kumbe tunapozimia mioyo yetu yeye hutupa nguvu mpya.

Sio kutupa nguvu tu, hutupa kustahimili yale magumu tuanayopitia katika maisha yetu ya kila siku. Na hatuachi tuanguke chini moja kwa moja.

Nikakumbuka mengi sana katika kutafakari Neno lake, kweli kuna wakati unafika unasikia kuchoka kweli kweli. Lakini yeye hutupa nguvu mpya za kuendelea mbele.

Tunapaswa kuona hili kwa upana wake, ikiwa Mungu anaweza kutupa kustahimili changamoto na kutupa nguvu mpya za kuendelea mbele. Tunazo sababu za kumrudia na kumtegemea yeye katika roho na kweli.

Hakuna jambo lingine linaweza kutupa tumaini kubwa kiasi kwamba ukiwa na gumu unapitia ujione u salama. Ni Yesu Kristo pekee ndiye wa kutegemewa katika hili, hakuna mahali sahihi tunaweza kupewa jambo kama hili.

Sijui unapitia jambo gani hapo ulipo, amini lipo tumaini njema kwako, ipo faraja ya kweli kutoka kwa Mungu aliye hai. Usitoke kwenye njia yake, endelea kung’ang’ana hapo hapo hata gumu unapitia.

Natamani uelewa kwa kina hili Neno la Mungu, huyu ni Mungu mwenyewe anasema na maisha yako siku ya leo.

Rejea: Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia. ISA. 40:29‭-‬31 SUV.

Binafsi unajua ni jambo gani limekufanya uzimie moyo wako, amini yeye anaenda kukupa nguvu nyingine mpya ya kuweza kufurahia maisha yako tena.

Ona kuinuka kwako tena kwa upya, iwe katika huduma, iwe katika familia, iwe katika masomo, iwe katika kazi, iwe katika biashara. Mungu anaenda kukuinua tena kwa upya ikiwa tumaini lako litakuwa kwake.

Haleluya, ni Neema ilioje kuona ulikuwa umechoka na kuonekana huna jipya tena, ila ghafla ukainuka tena kwa upya, na kwa nguvu mpya.

Sikia sauti ya Mungu ndani yako kupitia Neno lake takatifu, hii ni sauti ya kweli na halisi kwako.

Mungu akubariki sana.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081