“Salamu yangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni kufungwa kwangu. Neema na iwe pamoja nanyi”, Kol 4:18 SUV.
Tumezoea kuona mtu akiwa anapitia shida au changamoto fulani huacha kufanya mambo ya muhimu aliyokuwa anayafanya hapo awali.
Mtu anaona bora kupumzika au kuacha kabisa hadi pale atakapokaa sawa, jambo ambalo linaweza kumrudisha nyuma zaidi.
Zipo shida ngumu kama vile mtu kupata ukilema kwenye mwili wake, huyu anaweza kusimama baadhi ya mambo.
Yupo mwingine anaweza asiwe na kilema ila akawa anapitia kipindi kigumu katika maisha yake.
Wakati mtume Paulo amefungwa gerezani na Warumi mara ya kwanza aliandika nyaraka kwa Wakolosai, Filemoni, Waefeso na Wafilipi.
Nyaraka hizi tunazisoma hadi leo, nyaraka zilizojaa maonyo, maarifa na hekima mbalimbali kwa kanisa.
Pamoja na mtume Paulo kuwekwa gerezani kwa muda mrefu tunaona nyaraka hizi alizoandika zimejaa shukrani nyingi.
“Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo, siku zote tukiwaombea; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru”, Kol 1:3, 12 SUV.
Tunaweza kufikiri tukiwa kwenye kipindi kigumu cha uchumi, kukosa kazi, kupata hasara kwenye biashara, kukosa mtaji, kufukuzwa kazi, ndio kipindi cha kuacha kumtumikia Mungu.
Wengine tukiwa katika hali hiyo tunaweza kufikiri ni wakati wa kuacha kwenda kanisa, kuacha kusoma neno, kuacha kuimba, kuacha nafasi uliyokuwa nayo kanisani.
Mtume Paulo hakuacha kuandaa nyaraka mbalimbali akiwa Gerezani, akiwa kwenye maumivu mengi, tunamwona hakuwa na sababu ya kutofanya kile Mungu alimpa.
Ndugu mpendwa, tunahitaji kujitoa haswa, bila kujalisha hali tunazopitia, kama mikono na akili zako zinafanya kazi sawa sawa usiache kutumika kwenye nafasi yako.
Liwe jua iwe mvua jitoe kwenye kutumikia kusudi lako, acha visingizio, Mungu amekuamini, simama katika eneo lako la utumishi.
Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest