Zipo hatua katika maisha tunapokuwa huwa tunakuwa na utii sana mbele za Mungu, bidii ya kumtafuta Mungu huwa inakuwa kubwa sana.

Usikivu wa mtu huwa unakuwa wa kiwango kizuri kabisa, hata unapomtazama unamwona kabisa hana unafiki ndani yake.

Hili tunaliona hata kwa watu tunaoishi nao, wanaweza wakawa wafanyakazi wenzetu, wanaweza wakawa wafanyabiashara wenzetu, wanaweza wakawa ndugu zetu wa damu, wanaweza wakawa washirika wenzetu kanisani.

Wakati bado hawajafika hatua fulani ya mafanikio huwa wanakuwa wenyenyekevu sana kwa watu na kwa Mungu. Hata wale wasiomjua Kristo utawaona waliovyo na unyenyekevu kwa watu.

Lakini wapo watu Mungu atapowainua wakafikia mafanikio fulani ya kiwango kizuri, unamwona kabisa anabadilika tabia yake.

Alikuwa na unyenyekevu, ule unyenyekevu unatoweka ndani yake na kuanza kuonyesha tabia isiyo nzuri kwa watu na kwa Mungu.

Alikuwa mtu wa kupenda ibada ila baada ya kufanikiwa unaanza kumpata kwa shida sehemu za ibada. Ukimuuliza anaanza kutoa visingizio vingi visivyo eleweka sana kwa mtu aliyetolewa mahali na Mungu.

Alikuwa mtu asiyeweza kupitisha siku bila kusoma neno la Mungu na kutenga muda wa kutafakari yale aliyojifunza. Lakini baada ya kufanikiwa na kufika viwango fulani kiroho na kimwili, hilo jambo analiacha kabisa.

Alikuwa mtu wa maombi sana kabla ya kuoa/kuolewa, lakini baada ya kuoa/kuolewa ile bidii yake ya maombi haipo tena. Tena hata ile kiu haipo tena amebaki tu mkavu na kusimlia watu kuwa alikuwa vizuri zamani.

Kabla hajapata kazi ya kufanya alikuwa ni mtu anayempenda sana Mungu ila baada ya kupata kazi unamwona anabadilika, ule upendo/utii wake kwa Mungu unauona haupo tena kwa kutazama matendo yake.

Wakati ana washirika wawili alikuwa mtu mnyenyekevu sana na anayemtafuta Mungu kwa bidii, lakini baada ya Mungu kumletea washirika wa kutosha kanisani. Ghafla anabadilika na kuwa mtu wa tofauti kabisa.

Pamoja na hayo yote, uwe bado hujafanikiwa kabisa, ama uwe umeanza kufanikiwa, ama uwe umeshafanikiwa tayari.

Uwe upo kwenye kundi ambalo bado hawajamsahau Mungu, lipo angalizo lako au tahadhari yako hapa. Ili utakapoenda kinyume uwe na uhakika utarudi chini.

Rejea: Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; KUM. 8:12‭, ‬14 SUV.

Sijui kama umeelewa hiyo mistari miwili, naendelea kusisitiza kuhusu hili, moyo wako usije ukainuka ukamsahau Mungu wako aliyekufanikisha.

Kama hicho kiswahili cha kuinuka kitakuwa kigumu kwako, basi nakwambia usije ukawa na kiburi moyoni mwako ukamsahau Bwana Mungu wako.

Usije ukajichanganya na kujiona wewe ndiye mwenye akili nyingi sana kuliko wengine, usije ukaona nguvu zako ndio zilizokufanya ukafanikiwa na ukamsahau aliyekuwezesha kuupata huo utajiri, au kupata hayo mafanikio.

Rejea: Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo. KUM. 8:17 SUV.

Najua utafanikiwa ikiwa unabidii ya kazi na ukiwa umemtanguliza Mungu kwa kila hatua ya maisha yako. Usije ukawa kwenye kundi la watu ambao watakuwa hawana muda na Mungu tena.

Utakapofanikiwa hakikisha humsahau Mungu wako, mkumbuke siku zote za maisha yako. Maana ndiye aliyekupa mafanikio hayo unayoyaona kwa macho yako.

Rejea: Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo. KUM. 8:18 SUV.

Kuishi kwako kunaweza kukabadilika kutokana na hatua uliyopiga kimafanikio ila kumbuka siku zote aliyekupa huo utajiri ni Mungu, kumbuka aliyekupa hivyo viwango vya kiroho ni Mungu mwenyewe.

Usije ukasahau hili siku zote, kudumu kwa mafanikio yako ni kuendelea kunyenyekea mbele za Mungu. Kuendelea kuutafuta uso wake, kuendelea kupenda ibada.

Kufanya hivyo Mungu ataendelea kuwa rafiki yako siku zote za maisha yako, Mungu wetu sio kigeugeu, wala sio mwanadamu hata aseme uongo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com