Huenda umekuwa ukipata sana shida pale mtu anapotenda dhambi fulani, jamii inakuwa kama imemtenga hivi. Kwa kuchukulia mambo kawaida unaweza kuona hawatendi haki kufanya hivyo, kwa jinsi unavyotazama kwa mtazamo wako ulionao.

Tumekuwa tukiona makanisa mengi mtu akitenda dhambi ya wazi, mara nyingi hutengwa kwanza na kanisa. Wengi wetu tumekuwa tukichukizwa sana na hichi kitu, huwa tunaona wanafanyiwa isivyo haki.

Kwa kuwa mimi na wewe tumeamua kujifunza Neno la Mungu linavyosema, tunapaswa kukubali kupokea ukweli ulivyo. Tunapojua ukweli kupitia Neno la Mungu, hata mtazamo wetu unabadilika, vile tulivyokuwa tunafikiri zamani tunatoka kufikiri hivyo na kuanza kufikiri kwa namna nyingine tofauti.

Suala la kutengwa na kudharauliwa wenye dhambi halikuanza leo, Biblia inatuonyesha lilianza tangu agano la kale. Inatupa kujua jinsi gani dhambi ilimfanya mtu atengwe na wenzake, na Mungu wake.

Hili linatupa picha kwamba, dhambi ni jambo baya sana, sio baya tu, linatufanya tuonekane watu wasiofaa machoni pa watu wengine.

Unaweza kuwa shahidi wa hili, ukisikia mpendwa mwenzako amefumaniwa na mke/mume wa mtu. Utashangaa unaanza kumwona kwa mtazamo wa tofauti kabisa, unaweza kuanza kumwogopa utafikiri atakuua.

Unaweza kukosa marafiki ghafla kwa sababu ya dhambi, hata wakati wa shida yako unaweza kushangaa unaomboleza peke yako. Hata mtu wa kukutia moyo anaweza asipatikane kirahisi, chanzo nini, ni dhambi uliyofanya.

Mtu anaweza kuwa alikuwa anaheshimika sana kupitia huduma aliyompa Mungu ndani yake, siku amejulikana ametenda dhambi fulani. Huyu mtumishi heshima yake itaporomoka kuanzia siku ile ile.

Utasema sisi kama wakristo hatupaswi kufanya hivyo ila unapaswa kufahamu Neno la Mungu kwa wingi. Ili uwe na uwanja mpana wa kuweza kupambanua mambo mbalimbali.

Hili tunajifunza kupitia Yerusalemu, baada ya kumtenda Mungu dhambi ile heshima yake iliondoka. Wale waliouheshimu mji wa Yerusalemu, walianza kuudharau na kuonekana kitu kichafu.

Kabla sijakupa andiko linaloonyesha wazi hili ninalokuambia hapa, naomba ujitathimini mwenyewe huwa unasikiaje unapomwona mwenye dhambi ametengwa? Rudi na kwako, mtu uliyekuwa unamwamini na kumheshimu, ukisikia kashfa yake ya dhambi aliyofanya huwa unajisikiaje juu ya yule mtu?

Bila shaka kuna viwango utakuwa umemshusha sana, sasa kama wewe unafika mahali unamshusha viwango mtu uliyemwamini. Inakupaje shida unaposikia kanisa limemtenga fulani na kumfungia kushiriki meza ya Bwana mpaka pale atapofunguliwa tena.

Hebu tutazame maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hili;

Rejea: Yerusalemu amefanya dhambi sana; Kwa hiyo amekuwa kama kitu kichafu; Wote waliomheshimu wanamdharau, Kwa sababu wameuona uchi wake; Naam, yeye anaugua, Na kujigeuza aende nyuma. OMB. 1:8 SUV.

Umesoma vizuri huo mstari, unaonyesha wazi ni kiasi gani dhambi ilivyo sio nzuri. Utaona jinsi ilivyoifanya Yerusalem kudharauriwa na ile heshima yake kutoweka kabisa.

Usishangae leo ukitenda dhambi hata wale marafiki zako wa kiroho uliokuwa nao karibu, wanaanza kupukutika kidogo kidogo na mwisho unajikuta umebaki peke yako.

Usipoenda haraka mbele za Mungu kujipatanisha naye, utazidi kujichafua zaidi kwenye macho ya watu. Ipo gharama ya toba, na wote tunajua kutengeneza upya na Mungu inahitaji ujitoe haswa. Sasa usiporudi mbele Mungu, itakufanya uzidi kudharauliwa zaidi na zaidi.

Jitahidi sana kuwa na mahusiano mazuri na Mungu wako, usikubali ukakaukiwa na Neno la Mungu moyoni mwako. Ili usije ukamtenda Mungu dhambi kwa kupungukiwa na Neno lake.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.