Kugombana au kutofautiana sio jambo zuri, wala sio jambo la kumpendeza Mungu, unaweza kushangaa inakuwaje kukawa na faida katika kugombana kwa wawili wenye nia njema ya kuishi kama mume na mke.

Hata maandiko yameweka wazi kuhusu hili;

Rejea: Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. YAK. 3:16 SUV.

Kushangaa kwako kunaweza kukawa na maana nzuri kabisa, lakini kuna madhara usipojua kwanini kinatokea kitu ambacho hata wewe kuna wakati huwa kinakutokea.

Katika maisha yetu ya kila siku, kuna vitu huwa vinatupelekea tuchukie, hasa vinapotokea pale ambapo vinatuingiza katika hasara, au kukosana na Mungu wetu.

Kugombana hakuji hivi hivi, huwa kuna kisababishi cha kuwafanya wale watu wagombane. Unaweza ukawa ugomvi wa kawaida, na unaweza ukawa ugomvi mkubwa.

Ugomvi ule unaweza kusababishwa na wawili wale, ama kwa mmoja kukosa hekima, ama katika mazungumzo yao kunaleta kutofautiana. Katika kutofautiana huko kunaibua hasira inayopelekea ugomvi.

Kuudhiwa na kukasirishwa ni jambo ambalo linaweza kuwa ni gumu kuepuka, ukiwa duniani na ni mwanadamu ni jambo ambalo linatokea tu katika maisha ya mtu.

Tahadhari tuliyopewa wakristo ni kutotenda dhambi, yaani katika hasira yako jitahidi kutomtenda Mungu dhambi. Maana hilo jambo lipo ndani ya uwezo wako kuliepuka usitende dhambi.

Rejea: Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka. EFE. 4:26 SUV.

Hasira ndio hupelekea ka ugomvi humo, sasa hako ka ugomvi hakapaswi kumtenda Mungu dhambi. Kwa maana nyingine mnapaswa kuyamaliza na kusameheana.

Tahadhari nyingine iliyotolewa kwetu ni hii hapa, angalia hili andiko ninaloenda kukushirikisha hapa chini, uone pia hupaswi kuwa na hasira za haraka.

Rejea: Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu. MHU. 7:9 SUV.

Tumepata somo lingine hapo kuwa hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu, na sifa moja wapo ya mpumbavu ni ngumu kumbadilisha kwa kile anachoamini yeye hata kama cha uongo.

Mpumbavu hafundishiki, anachojua yeye ndio kile kile  hataki mtu mwingine ampandie kitu kipya. Sasa kama una mchumba mpumbavu na kuna tabia huipendi na imekuwa inakuumiza moyo wako. Hadi kufikia hatua mnakorofishana, huoni kuwa unapaswa kuchukua hatua?

Katika hali hiyo niliyokuelezea hapo, husaidia sana kumwelewa mtu, sio kumwelewa tu, zipo faida nyingi unazoweza kuzipata kama utautazama ugomvi wenu kwa njia ya kujifunza.

Nimekuandalia faida sita, zinaweza zikawa zaidi ya sita, ila hapa tutajifunza faida sita za kugombana na mchumba wako, au rafiki yako mliye na malengo ya kuja kuishi kama mume na mke.

Twende pamoja tuzione hizi faida sita za kugombana, au tunaweza kusema kutofautiana mitazamo, au jambo  fulani.

1. Unakuwa na muda zaidi wa kumwomba Mungu.

Kugombana kunaweza kuibua tabia njema kwa mchumba mmoja wapo, kupitia ugomvi wao wengi huwapelekea kuwa na muda wa kufunga na kuomba Mungu.

Kinachowafanya kufunga na kuomba ni ile hali wanayokutana nayo kwa wachumba wao, wanapata msukumo wa kumweleza Mungu kama mahusiano waliyonayo ni sahihi kweli au walikosea.

Mungu wetu ni mwaminifu sana, mtu akienda kwake kwa kumaanisha kweli na kuamini moyoni mwake. Lazima atamjibu, kama hayakuwa mahusiano sahihi utaona wametenganishwa, na safari yao kuishia hapo.

2. Unajua uhalisia wake ukoje.

Mnapokuwa kwenye urafiki au uchumba, mara nyingi sana watu wengi huwa huwezi kujua uhalisia wao. Labda itokee mlisoma pamoja kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, wakati ambao umejitambua na umekuwa na uwezo wa kupambanua mambo.

Sio tu kusoma shule moja, muwe mlikuwa majirani sana wenye uhusiano wa karibu sana, na hapa bado haitakupatia uhakika wa ulinaye ni chaguo sahihi.

Ndio maana unapaswa kumshirikisha sana Mungu, unaweza kumfahamu mtu kwa nje ila akawa na mambo yake ya siri. Ambayo kwa akili za kawaida huwezi kuyatambua kabisa hayo mambo.

Lakini tunapokuja kwenye suala la uchumba, kiasi fulani mtu anakuwa na ka uhakika wa kuwa aliyenaye ni chaguo sahihi kwake.

Pamoja na uhakika huo uchumba huwa ni kipindi cha  matazamio, wewe ni shahidi sio kila uchumba huwa unafikia lengo la kuoana.

Wachumba kugombana wakati mwingine naona mimi ni fursa kwao, kwanini nasema hivyo, ugomvi ule unaweza ukawa msaada kwao. Unaweza kumwondoa mmoja wapo kwenye usingizi mzito au upofu, na kutambua anayetarajia kwenda kuishi naye ni mtu wa namna gani.

Anapotoka kwenye usingizi huo mzito, kwake itakuwa ni habari njema. Maana atajua maamuzi aliyokuwa ameyafanya ni maamuzi sahihi, au sio sahihi kwake, kwa mtu anayetaka kuishi naye.

3. Mtu unayeenda kuishi naye ni wa namna gani.

Kila mmoja anaweza kujiweka katika mazingira ya upole, akaonekana ni mtu mtaratibu sana asiyependa makuu.

Lakini pamoja na kujiweka hivyo upo upande wa pili, ambao wengi huwa hawapendi kuuonyesha mbele za watu wasije wakasemwa vibaya.

Katika kugombana unapata nafasi ya kujua mtu unayeenda kuishi naye ni wa namna gani, huwa mtu wa kusamehe, au huwa mtu asiyesamehe.

Unapata nafasi ya kufahamu mahusiano yake ya zamani anayaona ni afadhali, na wewe ni mbaya zaidi? Pale pale anaweza kutamka jambo ambalo linaweza lisiwe zuri ila linakupa mwanga mtu uliye naye ni wa namna gani.

4. Unapata nafasi ya kujua vitu asivyopendezwa navyo.

Sio kila jambo unalolipenda wewe, mwenzako anakuwa analipenda, na sio kila jambo asilolipenda mchumba wako na wewe utakuwa hulipendi.

Anaweza kukueleza katika hali ya kawaida kuwa jambo fulani halipendi, usichukulie kwa uzito mkubwa sana moyoni mwako. Lakini anapoona humwelewi kwa kuendelea na lile alilokuambia, linaweza kuibua kugombana.

Hiyo itakusaidia sana kuepuka kufanya jambo asilolipenda, na hii inaweza kupelekea kuacha kabisa. Ama hii inaweza kukupelekea kuachana naye, sio kwa ubaya, unakuwa umeshajua huyo sio wa sawa yako.

Hii inawasaidia sana wale ambao wanaingia kwenye mahusiano yasiyo sahihi kwao kwa kukurupuka, huenda kilichowapelekea kuona ni mtu sahihi ni uchanga wao wa kiroho, na kutokuwa na maarifa sahihi ya neno la Mungu.

Unaweza kuona ni jinsi gani ugomvi unaweza kumfanya mhusika kujipima juu ya uamuzi wake kwa aliyenaye wakati huo, anamfaa au hamfai.

5. Unakuwa na utayari wa kuishi naye.
Sio kila wachumba wanaoenda kufunga ndoa yao kila mmoja wao anakuwa na utayari ndani yake. Wengi wanakuwa hawana uhakika sana na yule anayeenda kuishi naye.

Mtu anaingia kwenye ndoa akiwa ana mashaka mengi, au wasiwasi wa kutosha juu ya mwenzi wake. Huu wasiwasi ukienda kuleta majibu kama alivyokuwa anafikiri, uwe na uhakika hiyo ndoa haitakuwa na amani kama Mungu hataingilia kati.

Sasa katika kipindi cha uchumba ambacho huwa tunasema ni kipindi cha matazamio/maandalizi, maana uchumba huwa unaweza kuvunjika wakati wowote. Kunamsaidia mwanamke/mwanaume kuwa na utayari usio na mashaka mengi kwa mwenzake.

6. Unakuwa na maandalizi mazuri.
Hili kwa siku hizi linaweza lisiwe kipaumbele sana kwa wengi, kutojua unayeenda kuishi naye ni mtu wa namna gani. Huko ni kutokuwa na maandalizi mazuri.

Maandalizi ni pamoja na kufahamu unayeenda kuishi naye ni mtu wa namna gani, mfano kama ana mtoto aliyempata nje ya ndoa yenu. Je upo tayari kuishi naye, au ukifika kwenye nyumba yenu cha kwanza ni kuanza vita vya kutomkubali huyo mtoto.

Lakini kama hili jambo lilianza kuleta malumbano kabla ya kuoana, litakusaidia kuweka mazingira mazuri ya mtoto. Ama inakusaidia kujiandaa kiakili kuwa mwenzangu ana mtoto wake anayemhudumia.

Yapo maandalizi ya ndani ya moyo wako ambayo wengi huyasahau, na yapo maandalizi ya nje ambayo wengi huyaanda zaidi. Lakini yote ni muhimu hasa yale ya ndani ya moyo, unakuwa unajua unaenda kuishi na mwanaume/mwanamke wa namna gani.

Haya mambo muhimu sana kuyafahamu, wapo wanandoa wengi walienda kuwashangaa wenzi wao ndani, na kuona ilikuwaje wakakubali wakaoana nao. Wakati walikuwa na nafasi ya kuyatambua hayo wakiwa kwenye uchumba.

Utulivu na amani kwenye uchumba wenu hakukuhakikishii uzuri wa ndoa yenu, sio kila utulivu na amani kwenye uchumba unakuthibitishia usahihi wa mke/mume. Utulivu au amani zingine huwa feki.

Rejea: Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. 2 KOR. 11:14 SUV.

Hii inatuthibitishia wazi mtu mbaya anaweza kujificha kwa upole na kuonyesha ni mtu mzuri, ila nyuma ya pazia ana tabia ambazo sio za kuhimili kwenye ndoa.

Kumbuka, kugombana na mchumba wako sio kithibitisho cha mwisho cha uliye naye sio chaguo sahihi la Mungu kwako. Wakati mwingine ni uchanga wa mtu, au mtazamo hasi juu ya jambo fulani, lakini akieleweshwa vizuri anaelewa na kubadilika.

Mungu akubariki sana.
Mtumishi wa Kristo,
Samson Ernest
+255759808081