Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe hutaoa mke, wala hutakuwa na wana wala binti mahali hapa. Maana BWANA asema hivi, katika habari za wana, na katika habari za binti, wazaliwao mahali hapa, na katika habari za mama zao waliowazaa, na katika habari za baba zao waliowazaa, katika nchi hii; watakufa kwa maradhi mabaya; hawataliliwa, wala hawatazikwa; watakuwa kama samadi juu ya uso wa nchi; nao wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa; na mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi. Yer 16:1‭-‬4 SUV

Hapa nabii Yeremia anapewa ujumbe na Mungu kuwa asioe, wala hatakuwa na watoto, sio kana kwamba Yeremia alikuwa na shida ya kiafya, wala sio kana kwamba Yeremia aliamua mwenyewe asiwe na mke na watoto. Hili lilikuwa agizo la Mungu asifanye hivyo, hakutakiwa kufurahia maisha ya ndoa.

Sababu iliyopelekea Yeremia apewe maagizo ya kutooa ni kwa sababu Yuda ilikuwa inaenda kuangamizwa na Mungu mwenyewe kutokana na kosa walilolifanya la kuabudu miungu mingine, Yeremia alipewa maagizo mengine ya kutohudhuria msiba wowote, wala shughuli yeyote ya kijamii.

Wote tunajua katika jamii zetu za Kiafrika kutohudhuria matukio ya kijamii ilivyo na madhara makubwa, lakini YEREMIA alipigwa marufuku kutohudhuria misiba au sherehe yeyote, maana Mungu alikuwa anaenda kuangamiza nchi na miili ingezagaa kila kona, wala hawatazikwa na ingekuwa mbolea na chakula cha ndege wa angani.

Utaona kuwa Yeremia asingetii maagizo ya Mungu, alafu akaenda kuoa angekuja kubaki peke yake tena, angebaki na maumivu ambayo hayakuwa na sababu yeyote maana Mungu alishasema naye kabla. Alichotakiwa ni kutii na kufuata kile ameambiwa na Mungu.

Sasa tuangalie faida 5 za kumsikiliza Mungu anachokuelekeza ufanye/usifanye;

  1. Hutafarakana na Mungu.

Wakati mwingine tumefarakana na Mungu kwa sababu ya kutotii sauti yake au maelekezo yake anayotupa kupitia neno lake, tunaambiwa tusifanye jambo fulani tunapuuza na kulifanya lile ambalo tumekatazwa na Mungu tusilifanye.

Hapo tunakuwa tunakosea na kufarakana na Mungu wetu, ule uhusiano wetu mzuri tuliokuwa nao na Mungu unakuwa umepotea kutokana na kutomsikiliza yeye. Lakini tunapomsikiliza na kufuata kile alituambia tufanye au tusifanye, tunakuwa salama kabisa.

Uhusiano wetu unakuwa mzuri na Mungu, mahusiano yanapokuwa mazuri na maendeleo yetu kihuduma yanakuwa mazuri, unaweza kuona ni jinsi gani unapaswa kumsikiliza sana Mungu anapokuzuia usifanye jambo fulani hata kama kwako unaona ni zuri na la muhimu.

2. Hutaingia hasara

Zipo hasara nyingi tunaingia kwa sababu ya kutomsikiliza Mungu, unaambiwa usioe binti fulani ila kwa kuwa machoni pako anakupendeza na kukuvutia unaamua kuoa, baada ya muda mfupi kwenye ndoa unaanza kukutana na changamoto ngumu kwenye ndoa yako. Vile vile kwa binti unaambiwa usiolewe na mwanaume fulani, kwa kuwa amekuvutia na anakufanyia mambo mazuri unaamua kuolewa naye, baada ya kuingia kwenye ndoa unapata shida na kuachwa.

Huo ni mfano, ipo mifano mingi zaidi unayoweza kuingia hasara kwa kutomsikiliza Mungu wako, unajua kwenye hasara hakunaga shangwe na vigelegele, huwa ni maumivu na majonzi mengi ya kulia. Hii yote inaletwa na kutomsikiliza Mungu wako.

Unapomsikiliza Mungu unaepuka hasara nyingi kwenye maisha yako, hili ni la muhimu sana kulielewa na kulishikilia, na kama hujajua namna ya Mungu anavyosema na wewe, unapaswa kujifunza. Na kama unajua unapaswa kutumia hiyo nafasi ili kuepuka hasara.

3. Hutojuta katika maisha yako

Walimwengu walisema “majuto ni mjukuu” unapoacha kumsikiliza au kumtii Mungu utegemee kujuta kwenye maisha yako, na unapomsikiliza Mungu utegemee kutojuta kwenye maisha yako. Hata kwenye maamuzi yako, kama umejenga utaratibu wa kumsikiliza Mungu kwanza uwe na uhakika hutojuta kwenye maisha yako.

Mara nyingi tumejikuta tumeingia kwenye majuto kwa sababu ya kutotii au kutosikiliza maagizo au maelekezo tuliyopewa, hiyo imetuletea au imewaletea maumivu wengi wetu. Unahitaji kutii, haijalishi moyo wako unatamani, kama kipo kinyume na mapenzi ya Mungu kwa wakati huo unapaswa kuachana nacho.

4. Waliokudharau watamtukuza Mungu wako

Unaweza kudharaulika kwa kipindi fulani, watu wanaweza wasikuelewe maisha unayoishi kwa sasa, hasa ukiwa mwanafunzi, kuna tabia fulani unakuta wanafunzi wenzako wanazifanya kama jambo la fahari kwao.

Wewe ambaye huendani nao wanakuona huelewi mambo, upo nyuma ya dunia, unapitwa na mambo mazuri, wengine wanaenda mbali zaidi kwa kukuambia usipofanya hayo utayafanya ukubwani au ukiwa mzee. Hiyo yote ni kukutafuta kukushawishi uingie kwenye mitego mibaya.

Watu wanapoona umesimama na msimamo wako, uwe na uhakika watamtukuza Mungu wako siku moja, watasema hakika yule kijana ana Mungu, watasema hakikia yule mama/baba ana Mungu. Watasema hakika yule mtumishi ana Mungu anayeishi, nini wameona kwako? Ni ule msimamo wa Kimungu uliokuwa nao bila ya kuyumbishwa na upepo wowote.

5. Utaheshimika zaidi ya mwanzo

Wakati mwingine huwa hatuoni heshima sana tunapokuwa wana wa Mungu, watu wanaompenda Mungu na kuishi vile anataka yeye, vile tunafuata mapenzi ya Mungu kuliko ya kwetu. Watu hutuona watu waliopoteza mwelekeo fulani, watu wasio na akili.

Inapofika wakati matunda ya kazi zetu au huduma zetu zinaanza kuzaa matunda au kutoa matokeo mazuri huwa heshima inaanza kuonekana kwetu. Watu hutuona na kutuchukulia kwa namna ya tofauti kabisa na mwanzo.

Mwanzo walituona hatuna lolote ila inapofika wakati wetu wa kubarikiwa mambo ya mwilini, huanza kutuchukulia kwa heshima kubwa kuliko mwanzo. Hii yote ni matunda ya kumtii Mungu maelekezo yake aliyokupa.

Tofauti na mtu anayeanza huduma anataka mafanikio makubwa kwenye huduma yake kwa muda mfupi, tena mafanikio ya kimwili, huyu hatafika mbali akiwa anamtumikia Mungu wa kweli. Na heshima zao huwa za muda mfupi na inayofuata ni aibu kubwa kwenye maisha yake, hii kataa kwako, msikilize Mungu utaona faida yake.

Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo, heri mwisho wako uwe na heshima kubwa kuliko mwanzo wako wa aibu na kuchekwa sana. Utafurahia maisha sana mwanzo na kupata heshima kubwa ya bandia alafu mwisho ukawa na aibu kubwa, hii ni hasara kwako usikubali kabisa.

Mwisho, soma neno la Mungu likujenge kimwili na kiroho, hii iwe tabia yako ya maisha, kama unapenda kuungana na wenzako wanaosoma neno la Mungu kila siku, ungana nasi kwenye kundi la wasap kupitia namba hii +255759808081. Tuma ujumbe wako kupitia hiyo namba utaungwa kwenye kundi.

Mungu akubariki sana.

Samson Ernest

+255759808081