Haleluya,

Kuna hali huwa tunapita wana wa Mungu mpaka tunaanza kujiuliza labda tumekosea wapi, huwa tunaanza kujihoji huenda kuna eneo tumekosea.

Tunaweza kuona ndugu na marafiki wamekuwa mwiba kwetu, kwa jinsi wanavyotutendea mambo mabaya juu yetu. Kumbe ndio daraja letu la kupandishwa juu zaidi, kutokana na mambo mabaya waliyotutendea.

Tunaweza kuona majaribu/changamoto zinatuandama sana kwenye safari yetu ya mafanikio, kumbe majaribu hayo makali yanatupeleka kwenye furaha kuu.

Tunaweza kuona kazini kwetu majaribu yamezidi sana kila unachofanya unaona ni cha moto, kumbe ndio nafasi yako unaandaliwa kwenda kwenye nafasi fulani nzuri zaidi.

Kufikiri kwetu kibinadamu kunaweza kutufanya tufikiri Mungu ametuacha, tunaweza kufikiri kuna mahali tumemtenda Mungu dhambi ndio maana anaruhusu mapigo juu yetu.

Unapofika wakati wa kuinuliwa ndio unakuja kujua kweli hii njia haikuwa ya mateso ya hasara. Yalikuwa ni mateso ya faida, maana muda mwingine shetani anaweza kujichukulia sifa kutokana na mateso unayopitia. Bila kujua hayo mateso makali yana mpango maalum wa kukufikisha kwenye mazingira ya kustarehe.

Nakueleza vitu halisi vilivyo ndani ya biblia yako, huenda ulishaanza kufikiri kuacha wokovu kwa sababu umeona majaribu yamezidi. Nakusihi usije ukaacha WOKOVU kwa sababu ya changamoto zimekuwa kama moto unaochoma.

Mungu anakuandalia kitu kizuri katikati ya mateso yako, sio mimi nasema ni Neno la Mungu linasema;

Rejea: Uliwapandisha watu Juu ya vichwa vyetu. Tulipita motoni na majini; Ukatutoa na kutuleta kunako wingi. ZAB. 66:12 SUV.

Hili andiko huenda usione uzito wake vizuri kutokana na tafsiri yake, ila ngoja tujaribu kuangalia kwenye biblia nyingine ya kiswahili cha kisasa.

Rejea: Uliwaruhusu watu watukalie vichwani, tulipita kwenye moto na kwenye maji, lakini ulituleta kwenye nchi iliyojaa utajiri tele. Zaburi 66:12 NEN.

Hawa ni wana wa Israel wanaeleza yaliyowapata, kisha wakajua kumbe yale magumu yaliyokuwa yanawatesa yalikuwa yanawasukuma mbele kuelekea kwenye nchi iliyojaa utajiri.

Huenda hapo ulipo unajiona umefika sehemu sahihi ila Mungu akitazama miaka mitano ijayo anakuona kwenye mateso makali zaidi. Kuona hivyo anaanza kukutengenezea mazingira mazuri ya mbeleni, haijalishi utaumia sana wakati wa kuelekea kwenye kilele cha mafanikio yako.

Ukiwa mwaminifu mbele za Mungu, uwe na uhakika Mungu yupo pamoja na wewe mguu kwa mguu, unyayo kwa unyayo. Iwe usiku au iwe asubuhi au iwe mchana au iwe jioni, amini Mungu yu pamoja nawe.

Kweli tunapita katika mateso makali, amini utafurahi siku moja, kikubwa usimwache Yesu Kristo, hakikisha uhusiano wako na Mungu hauondoki.

Wapo watu wanaweza kufikiri wanatunyonya na kuua ndoto zetu, kumbe wanatumika kama daraja letu la kutufikisha katika nyumba ya mafanikio.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
www.chapeotz.com
+255759808081.