Huna muda mwingine tena wa kuja kufanya jambo lolote lile baada ya maisha haya duniani kupita.
Haijalishi kuna jambo unalipenda sana, liwe baya au zuri, fahamu mwisho wake ni hapa duniani.
Haijalishi kazi unayoifanya inakupa heshima Kubwa sana, fanya kwa bidii maana baada ya safari yako kumalizika hapa duniani. Hutoifanya tena wala hutopewa heshima ya uongozi wako.
Leo kijana, tumia ujana wako vizuri kwa nguvu zako zote kufanya mambo yako vizuri ili siku ya kuondoka duniani uache alama njema. Maana hakuna nafasi nyingine tena ya kwenda kufanya hayo uliyokuwa unayatenda hapa duniani.
Hutaki kuokoka na unafanya uovu mwingi, fanya ukiwa duniani, baada ya kufa, hakuna nafasi nyingine tena ya kutenda uovu wako. Uchague mwenyewe kati ya maisha ya muda mfupi ambayo ni sasa, au uchague kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ambayo unaenda kuyaishi milele baada ya haya.
Unatumika Kwenye kiti cha utumishi wa Mungu, tumia nafasi hiyo kwa nguvu zako zote. Maana hakuna nafasi nyingine tena ya kwenda kutumika huko uendako.
Yapo mengi sana ambayo Mungu amewajalia watu wake kuwa nayo, angalia lipi ambalo linampendeza Mungu. Lifanye kwa bidii zote, maana ukishakufa na habari yako imeishia hapo.
Mungu akusaidie utende mema wakati u ngali hai, hakuna nafasi nyingine tena ya kwenda kutenda hayo unayoyatenda sasa.
Kuoa na kuolewa, kunafanyika tu hapa duniani, baada ya kufa, hakuna kuoa wala kuolewa tena. Kama ni kumpenda mke/mume wako, mpende sana sasa hivi bila kubakisha kitu.
Akishakufa huyo mke/mume wako hakuna upendo tena, maana huwezi kusema nampenda marehemu wakati hajui chochote.
Kama ni Neno la Mungu, soma sana sasa hivi. Baada ya kufa hakuna tena habari za kwenda kusoma Neno la Mungu.
Rejea: Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe. MHU. 9:10 SUV
Kwa kuwa umeokoka, chagua jema moja ulifanya kwa ufanisi mkubwa, ikihitajika nguvu zitumie haswa. Na ikihitajika akili zako zitumie haswa ipasavyo.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081