
Yesu asifiwe, siku nyingine tena Bwana ametupa nafasi ya kuifikia. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa nafasi hii.
Mtoto unaweza ukamkataza kitu na akaona unamwonea, wakati wewe unaona madhara ya hicho kitu. Yeye anakuwa anaona kizuri kwake.
Kwahiyo unaweza kupambana kumkataza kitu ila ukijisahau kidogo au ukawa haupo karibu naye. Utamkuta amerudia kufanya kile kile ulichomkataza.
Sio watoto tu ndio wanakatazwa vitu fulani na wanafanya, hata watu wazima yapo mambo tunakatazwa kuyafanya na tunafanya. Kwahiyo shida ipo pale pale kama ya watoto wadogo.
Sio kana kwamba hatuna akili, wakati mwingine tunakuwa hatujui madhara ya kile tunafanya au tunataka kufanya. Kwahiyo mtu anapotokea kutukataza kitu huwa tunaona anatuingilia maisha yetu.
Japo kuna mambo unaweza ukakatazwa ila yakawa hayana madhara kwako, isipokuwa anayekukataza anakuwa anafanya hivyo kwa hila na kwa manufaa yake binafsi.
Kukueleza hivyo nataka uwe na muda wa kufikiri, kwanini jambo fulani unakatazwa wewe? Huenda hapo ulipo kuna kizuizi umewekewa, unafikiri kwa sababu ya wivu watu? Au kwa sababu ambazo ni sahihi kabisa.
Bila kujipendelea kama umejua unachokatazwa ni kwa nia njema unapaswa kuwa mkweli, na kama huelewi kwanini unakatazwa pia unapaswa kuwa mkweli na kutafuta sababu.
Usisubiri madhara yatokee kwa kitu ambacho ulikuwa na muda wa kutosha kuepukana nacho. Wakati ulishaonywa mara nyingi, ulishashauriwa sana, kupata muda wa kutulia na kufikiri itakusaidia sana.
Kuwa mtu wa kufikiri kwa kina, pale mawazo yako yanaishia mruhusu Mungu mwenyewe ahusike ila wewe utakuwa umefanya sehemu yako.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com