Ili siku yako iishe kwa ushindi, uone moyoni mwako kuwa siku ya leo imepita vizuri na kuna kitu umefanya cha maana sana.

Vitu gani huwa ukifanya unajisikia vizuri moyoni mwako, hata kama kwa kujilazimisha kufanya jambo ambalo mwili wako hutaki kabisa siku hiyo.

Lazima kuna vitu ambavyo tukivifanya huwa tunajisikia vizuri, tunaona siku yetu tumeimaliza kwa ushindi mkubwa sana.

Inaweza ikatokea mtu asijue ni vitu gani vinamletea furaha ya moyo wake, au vinamfanya ajione ni mshindi kwa kuvifanya siku husika.

Napenda kuzungumza na wewe ambaye ukifanya vitu fulani huwa unajiona hujapoteza siku yako bure, ambavyo huwa unaona umefanya jambo la kukufikisha kwenye ndoto yako.

Mfano, siku yako ili iende au iishe vizuri ni lazima usome neno la Mungu. Hii imekuwa ni sehemu ya maisha yako, siku kuisha bila kusoma na kutafakari neno la Mungu unaona kuna kitu kimepungua katika siku yako.

Kutofanya hivyo utaona kabisa siku yako haina ushindi mkubwa sana, unaweza kutafuta sababu za kujitetea ila ndani ya moyo wako unaona kabisa kuna kitu hujakifanikisha siku hiyo.

Huo ni mfano, hebu na wewe fikiri ni jambo/mambo gani huwa yanakufanya uone siku yako imeisha kwa ushindi mkubwa. Na ukishayafanya huwa unajisikia vizuri hata kama ulikuwa umechoka sana siku hiyo.

Ukishayapata hayo mambo jiweke vizuri, mwombe Mungu akutie nguvu wakati unajisikia kuchoka, wakati unajisikia kukata tamaa. Ili ufanye bila kuacha.

Kujiwekea nidhamu ya kufanya kile umejiweka utaratibu wa kukifanya, nidhamu hiyo itakuzalia matunda makubwa sana. Hata kama kwa sasa unaona ni jambo dogo au la kawaida au mateso kwako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255759808081