
Katika maisha yetu haya, bila shaka umewahi kukumbwa na hali ya kumchukia mtu fulani aliyekuumiza au aliyekutenda jambo baya.
Wapo wengine tumewahi kujikuta au tumejikuta tunawachukia kwa kuambiwa na watu wengine. Bila kuwa na uhakika na taarifa tulizopewa, tunajenga chuki juu yao.
Leo napenda ujifunze jambo hapa, ujumbe huu utakufikirisha kwa kina zaidi ili usiwe kwenye kifungo kinachokutesa kwenye maisha yako kwa muda mrefu.
Hebu nikuulize, unaweza ukawa ni wewe au usiwe ni wewe mwenye changamoto hii ya kumchukia mtu fulani. Hilo lisikuzuie wewe usijifunze jambo la kukusaidia katika maisha yako.
Hebu jiulize una uhakika kweli hicho kinachomfanya umchukie huyo mtu ni kweli amekifanya au umeambiwa au umemhisi tu.
Tulia ufikiri kama ni kweli amefanya hupaswi kuendelea kumchukia, bali ona kwa mtazamo chanya kuwa utakuwa umeshajua tabia ya huyo mtu. Hapo umeshajua huyo mtu ni wa namna gani na unapaswa kuishije naye.
Kama umeambiwa na mtu kuhusu hayo aliyokuambia, umejithibitishia vipi kuhusu hizo taarifa. Ama umeishia kusikiliza shutuma za upande mmoja na ukamwona huyo mtu ni mbaya.
Na kama umehisi huyo mtu ni ndio chanzo cha wewe kuingia kwenye shida au ndiye aliyeleta madhara yote hayo. Unafikiri kuhisi kwako ni sawa? Na kama sio yeye ni mtu mwingine kabisa, na wewe unamhisi yeye, je hapo unaona ipo sawa?
Vizuri kufikiri na kutengeneza hoja za kukusaidia wewe kuchukua hatua ya kuweza kujiepusha na dhambi ambazo zitakutenga na Mungu.
Fikiri hii ya leo ipanue mipaka yako ya kufikiri zaidi, usiwe kwenye kachumba kadogo kanachokuzuia kuona mambo kwa mapana zaidi.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255759808081