
Kuna vitu huwa tunavifanya utafikiri kuna shida imetokea kwenye fahamu zetu, kumbe ni wazima kabisa wa afya njema.
Mtu anakujia kwako akiwa na shida kabisa, wakati mwingine anatoa na machozi kabisa. Unamhurumia na kumsaidia kile kiasi alikuwa anahitaji kutoka kwako umwazime kwa kukuahidi atakurudishia siku/mwezi fulani.
Unafika ule wakati ambao alikuahidi kwa kinywa chake, ukipiga simu hapatikani, akipatikana anakudanganya muda fulani atakuwa amekupa kiasi chako.
Muda huo unafika huoni matokeo yeyote, inaanza kazi ya kuzungushana kila siku, njoo kesho nitakupa unaenda hupati kitu, nipigie kesho nitakuwa nimeshapata unafanya hivyo humpati hewani.
Hebu fikiri wewe mwenye tabia kama hii, inawezekana umemgeuka yule aliyekuazima fedha zake. Je unafikiri amekosea kukupa? Na kama amekosea si ulikuwa na shida akakusaidia shida yako?
Fikiri tu mwenyewe unachomfanyia mwenzako aliyekusikiliza na kukupa fedha yake, huenda siku hiyo alikuwa na kazi nayo ya muhimu ila kutokana na uzito wa jambo lako. Akawa amekuonea huruma na kukusaidia ili uepukane na adha hiyo.
Kama umefikia hatua ya kumwambia ulikuwa na shahidi gani wakati unanipa hiyo fedha yako. Unafikiri Mungu anaweza kukuacha hivi hivi kwa kitendo kiovu ulichomfanyia mwenzako?
Hata kama utachukia nakuambia ukweli, huo sio usitarabu/uungwana uwe hupokei simu ya anayekudai, uwe umemwambia afanye chochote anachoona yeye, uwe umemwambia humlipi pesa yake na afanye anachotaka.
Nakueleza ukweli yale maumivu na machozi unayompa mwenzako yakimfikia Mungu huwezi kuwa salama kabisa.
Fikiri isingekuwa msaada aliokupa ungefanyaje siku hiyo wakati ulikuwa umetingwa kweli, na huenda ulizunguka kila mahali kuomba msaada kwa watu uliowaamini wanaweza kukusaidia wakawa hawana.
Acha hiyo tabia kabisa, kuwa mstarabu, huna wakati huo mweleze vizuri, tena usimweleze maelezo ya juu juu. Wala usisubiri akutafute yeye, na wala usidanganye kwa chochote, kufanya hivyo utakosea sana.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255759808081