Kila mmoja wetu kuna vitu anatamani viwe sehemu ya maisha yake au anatamani avifikie au avipate. Katika kutaka kuvipata anakuwa anapambana kufikia kile anakitaka.

Katika kupambana huko anashangaa lile alilolikusudia kulipata linaenda kwa mtu mwingine au halioni kabisa limepotelea wapi.

Mungu wetu ni mwema Sana, unaweza ukalaumu sana kwanini hukupata kile ambacho ulikitaka/ulikitarajia kiwe sehemu ya maisha yako.

Kulaumu kwako hakuwezi kubadilisha kile kimetokea, na kama utataka kulazimisha na mapenzi ya Mungu hayakuwa hivyo. Ujue unatafuta mengine kabisa ambayo mwisho wake huwa sio mzuri sana.

Kama utakuwa umeshajua haikuwa mpango wa Mungu, ukatulia na ukaendelea kumtumaini Mungu kwa kile unatamani kiwe chako.

Utakuja kushangaa anakupatia mahali pengine kabisa, au lile uliona linakufaa wewe kwa wakati huo, au kile ulikiona wewe kingekufaa kwa wakati huo, unakuja kupewa kilicho bora zaidi ya kile ulikuwa unataka.

Kufikiri kila jambo unalolikosa ni hila za Shetani huko unakuwa unakosea wakati mwingine, yapo mambo hutakaa upate kama wakati wa Mungu hujafika.

Na kufikiri kila unalolitaka wewe litakuwa la kwako kwa wakati unaoutaka wewe huko napo utakuwa unawaza vibaya. Muhimu ni kuruhusu Mungu mwenyewe afanye apendavyo kwa wakati wake.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com