Tunaweza tukawa watu wazuri sana wa kuwalalamikia wengine kwa kufanya mambo yasiyofaa, mambo ambayo ni chukizo kwa Mungu wetu.

Ninachoweza kukuambia leo, katika hilo unaloona halipo sawa wewe kama wewe umehusika vipi kuhakikisha kitu kama hicho hakitokei.

Elimu gani umeitoa kuhakikisha hicho kilichotokea hakitokei kwa mtu aliyepita kwenye mikono yako au kwenye ushauri wako? Kipi haswa umehusika nacho kwa sehemu yako uliyojaliwa na Mungu kuhakikisha unasaidia wengine.

Nakufikirisha tu, kabla ya kuanza au badala ya kuendelea kulalamika juu ya hicho unachokilalamikia, umehusika vipi kuepusha hicho kisitokee.

Inawezekana unalalamika mtoto wako ana tabia mbaya sana, ulihusika vipi katika malezi yake. Muda wako kwa mtoto katika kumfunza tabia njema, una uhakika uliutoa kisawasawa kwake?

Hao washirika unaowalalamikia wanakimbilia huduma za watumishi feki wanaotumiwa na Shetani. Umehusika vipi kuwafanya watambue Mungu waliyenaye ni mkuu kuliko huko wanakokimbilia hovyo.

Kingine umehusika vipi kuleta hayo matatizo, una uhakika mikono yako ni safi katika hilo lililotokea? Hakuna eneo umeleta uzembe katika nafasi yako uliyonayo?

Fikiri vizuri kama kiongozi, kama mzazi, kama mtoto, kama mwana wa Mungu, kama mtu aliyempokea Yesu Kristo, utagundua vitu vingi sana vya kujisahisha.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com