Nikizungumza mitandao ya kijamii sio jambo geni kwenye masikio yetu, ni jambo ambalo linaeleweka kwa watu wengi sana.

Hata yule ambaye hatumii hii mitandao ya kijamii anaijua, watu wengi sana ananunua simu anatamani awe mmoja wa wale waliopo Facebook, instagram, WhatsApp, Twitter, LinkedIn, YouTube nk.

Napenda nikufikirishe leo, tangu umejiunga au tangu umeifahamu mitandao ya kijamii, je imekusaidia nini tangu uanze kuitumia?

Kipi unajivunia kuhusu mitandao ya kijamii, kipi unaweza kumshuhudia hata mzee wa miaka ya kutosha akakuelewa.

Kipi unaweza kumshuhudia mwanao na akaona kweli mzazi wangu ana kitu alichokipata kupitia mitandao ya kijamii.

Ama kwako mitandao ya kijamii ni sehemu ya kupoteza muda wako, upo kwenye magroup ya wasap kama 20 hivi na huna unachofanya zaidi ya kuchati.

Akaunti zako zinatumika kukusaidia nini katika maisha yako ya kiroho na kimwili, kipi unaweza kujivunia leo na watu wengine wakahamasika na hicho ulichokivuna.

Ama kwako mitandao ya kijamii imekuwa tiketi ya kukupeleka jehanamu, ama imekuwa gereza la muda wako mwingi unatumika vibaya na kazi zako zingine unashindwa kufanya kwa ufanisi.

Kwenye huduma yako mitandao ya kijamii imetumika kueneza injili au imetumika kupoteza muda kwako. Ukiwa kama mtumishi wa Mungu unapata muda wa kuandaa somo la kufundisha kanisa au unadhurura tu masaa yote kwenye mitandao.

Hebu fikiri, kipi unajivunia kuhusu mitandao ya kijamii, maana wapo watu mitandao ya kijamii ni shule kwao, au wengine ni chuo kwao, na wengine ni biashara kwao, Sasa kwako mitandao ya kijamii ni nini kwako?

Kaa chini leo ufikiri, maana ukweli unaufahamu wewe jinsi unatumia mitandao ya kijamii, wala huhitaji kwenda kuuliza kwa mtu mwingine.

Ukishaona hakuna cha maana sana unapata au unafanya kwenye mitandao ya kijamii, nakushauri uchukue hatua sasa, ifanye mitandao ya kijamii kuwa faida kwako, iwe ya kiroho au kimwili, hakikisha unafanya hivyo.

Unapenda kupata hizi fikiri kuanzia sehemu ya kwanza kabisa, ingia kwenye link hii hapa utazipata zote=>>https://bit.ly/2uihjWk

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81