
Sio Mara zote kutojisikia vizuri au kutojisikia amani moyoni ni kwa sababu kuna watu wamekukosea. Sio kana kwamba umepewa taarifa mbaya, sio kana kwamba umekosa kazi, au fedha.
Wakati mwingine hatuna amani mioyoni mwetu kwa sababu ya kuchezea muda wetu vibaya katika siku yetu tunayopewa na Mungu.
Wakati mwingine ni kwa sababu ya kutowajibika vizuri kwenye eneo la kazi, au kwenye nafasi zetu.
Ukitaka kuamini hichi ninachokueleza hapa, kama kuna siku umewahi kumaliza mapema majukumu yako ya siku. Ndani yako huwa unajisikia vizuri sana, na unajiona mshindi siku hiyo.
Unakuwa huna hatia ndani yako, amani inakuwa kubwa kiasi kwamba watu wanakuwa wanakushangaa imekuwaje hadi unakuwa hivyo. Na wengine wanaanza kutamani kusikia nini kimekufanya uwe na furaha.
Ukitaka kukubaliana na mimi kuhusu hili, siku hujawajibika vizuri kwenye eneo lako au kwenye nafasi yako. Utaona mambo hayajakaa vizuri kabisa, unaweza ukakosa amani kabisa moyoni mwako.
Hili linaweza kueleweka vizuri zaidi kwa wale watu wanaowajibika vizuri kwenye nafasi zao, wale ambao hawajali sana au hawawajibiki kwenye nafasi zao wanaweza wasinielewe sana ninachosema hapa.
Kuondoa hali ya kuvurugika ndani yako, jitahidi kufanya kile ambacho ulipaswa kukifanya katika siku yako husika. Tena wakati mwingine hujisikii kufanya, unapaswa kujilazimisha kwa nguvu, utaona siku yako imeisha kwa ushindi mkubwa sana.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
Mtenda kazi katika shamba la Bwana.
+255 759 80 80 81
www.chapeotz.com