Kitu kinapozidi kuwa changamoto kwako, inabidi ukae chini na ujiulize nini inakupelekea kuwa hivyo. Hii itakusaidia kurekebisha pale unapoona ndio chanzo ya yote.

Ikiwa kwako changamoto kubwa ni kutojiamini, unapaswa kukaa chini na kufikiri nini huwa inakufanya usijiamini.

Labda hujiamini kusimama mbele za watu, labda hujiamini kuongea mbele za watu kuwaeleza kile ambacho unatamani wakisikie kutoka kwako.

Labda huwezi kumwelezea mteja wako uzuri wa bidhaa unayouza, kwa sababu ya kutojiamini kwako. Unafikiri ukimweleza hatakuelewa vizuri.

Kutojiamini kwa mtu kunaweza kusababishwa na mambo yafuatayo;

1. Nguo/Mavazi; kuvaa nguo ambayo moyoni mwake anajiambia/anajishuhudia sio nguo nzuri, na haina hadhi ya kusimama mbele za watu.

Ama mtu anamjia anaitoa kasoro nguo yake, na hiyo kasoro anaiona na kuikubali moyoni mwake, hii inamfanya mtu awe anajishutukia na ule ujasiri wake unatoweka kabisa.

SUHULISHO; Ili uweze kuepukana na hili unapaswa kuvaa nguo ambayo umeikagua na huna wasiwasi nayo. Pia unapaswa kuvaa nguo inayoendana na mazingira husika.

Nguo ambayo haitakuwa na maswali kwa watu, nguo ambayo haitakuwa kituko cha kila mtu kukushangaa na kukuona kituko.

Mfano; nguo ya shambani usivae kwenye tukio maalumu kama vile siku ya ibada, au sherehe, au ofisini.

2. Dhambi; dhambi ina mchango mkubwa sana ya kumfanya mtu asijiamini, dhamira ikiwa inamshitaki ndani yake, anaweza akaona kila mtu anajua alichofanya.

Mbaya zaidi awe alikutana bahati mbaya na mtu ambaye anafahamiana naye maeneo ambayo alitenda hiyo dhambi.

Anaweza kufikiri mambo yake yamekuwa wazi, kumbe hata huyo mtu hakujua chochote na alikuwa na mambo yake. Ila mshtuko na wasiwasi alionyesha kwa huyo mtu, umemfanya huyo aliyemwona apate maswali na wakati mwingine kutaka kujua zaidi.

SULUHISHO; Unapotenda Dhambi, badala ya kuendelea kujihukumu ndani yako na kuanza kufikiria watu wengine vibaya. Chukua hatua ya kutubu na kutorudia kosa hilo, hii itakufanya kuwa huru ndani yako na kuondoa wasiwasi ndani yako.

3. Familia Duni; hii inaweza ikawa sababu mojawapo ya mtu kutojiamini, yeye binafsi anakuwa ameshajinyanyapaa ndani yake na kujiona si kitu.

Wakati mwingine watu wanakuwa hawana habari na hicho anachokiwaza, watu wanakuwa na hamu ya kusikiliza kile anataka kusema. Kutokana na kuwa na wasiwasi mwingi, inamfanya kukosea mara nyingi.

Anapoanza kukosea, ama anapozungumza kama mtu asiye na uhakika na kile anachosema. Inawafanya wale wanaomtazama na kumsikiliza kuwa na mashaka naye, na kuondoa usikivu wao kwake.

SULUHISHO; Ikiwa Mungu amekupa kitu ndani yako, usisumbuliwe na maisha duni ya familia yako au ya kwako binafsi, kile ulichonacho kitoe kwa ujasiri na kwa usahihi. Hata kama watu hao wanakufahamu vizuri, ikiwa hicho kitu ni cha kweli.

Utaona watu wakihama kwenye eneo lile wanalokufahamu kama mtu usiye na kitu, na kukuona mtu wa tofauti uliyebeba kitu kikubwa sana cha kiMungu.

Hayo ni mambo machache yanayoweza kumfanya mtu asiweze kujiamini, yanaweza kuonekana ni madogo ila yanaweza yakawa ni tatizo kubwa kwa mtu.

Nimekupa suluhisho lake kuweza kushinda hiyo hali, ukiamini na kuweka katika matendo utaona mabadiliko chanya katika maisha yako.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest.
+255 759 80 80 81.