
Zipo nyakati ngumu mtu anakuwa amepitia kwa muda mrefu, nyakati ambazo wakati mwingine mtu anakuwa amekosa matumaini ya kuondokana na hali ile aliyonayo.
Anapokutana na muujiza wake, akaondokana na lile ngumu alilokuwa nalo, maisha yake yakabadilika ghafla, alikuwa haoni akaona, alikuwa hatembei akatembea, alikuwa hawezi kuongea akaongea, alikuwa hana mtoto akapata mtoto, furaha yake inaweza ikawa kubwa kupitiliza.
Maana saa ya Mungu inapofika kwa mtu, shida zake zote huondoka sasa ile ile, haijalishi hiyo shida watu walisema atakufa nayo, wala haijalishi watu walimwonaje. Saa ya Mungu inapofika kila kitu hubadilika kwenye maisha yake.
Mtazamo na namna ya kuwaza huwa tofauti kabisa saa inapofika kwa mtu, watu wengine hubaki wanashangaa wenyewe. Hakuna mtu ataacha kusema neno juu ya kile amekiona kimetendeka kwa mtu waliyemfahamu ana shida fulani, ghafla huyo mtu amekuwa mzima.
Furaha ya kuponywa kwa mtu, haiwezi kuzuilika, haijalishi mtakereka kiasi gani, lakini furaha ya mtu aliyetendewa muujiza na Mungu, mtu aliyemwona Yesu Kristo amemtendea jambo. Hawezi kunyamaza, wala huwezi kumzuia asipige kelele za shangwe.
Atafanya kila analoliweza kumsifu Mungu wake kwa matendo makuu aliyomtendea katika maisha yake, watu wengine msiojua nini kimepata mtu yule. Mnaweza kuendelea kushangaa na kuona ni nini kinaendelea kwa mtu yule.
Rejea: Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu. Watu wote wakamwona akienda, akimsifu Mungu. Wakamtambua, ya kuwa yeye ndiye aliyekuwa akiketi na kuomba sadaka penye mlango Mzuri wa hekalu; wakajaa ushangao wakastaajabia mambo yale yaliyompata. MDO 3:8-10 SUV.
Mtu aliyeponywa kweli, mtu aliyejibiwa maombi yake, huwezi kumzuia furaha yake. Hili tunajifunza kwa kiwete huyu tuliyesoma habari zake, huyu hakupata ukiwete wake ukubwani, tangu kuzaliwa kwake alikuwa kiwete.
Siku anapokea uponyaji wake, hakuangalia nini kinaendelea hekaluni, yeye aliingia ndani kwa kuruka-ruka na kumsifu Mungu wake. Hapa kama ni ibada kanisani utaratibu uliharibiwa na watu wakageuka kumshangaa ni kitu gani kimemwinua yule kiwete.
Furaha ya mtu mwingine inaweza kukukera, ila zipo furaha nyingine badala ya kukereka wewe, utakuwa mtu wa kusambaza habari za matendo makuu ya Mungu. Maana ulichokiona kimetendeka kwa mtu yule unayemfahamu, kinaweza kukufanya ukawa msambaza habari mwenyewe.
Kama unataka kuona hili jambo halina ustarabu sana, Mungu akutendee jambo ambalo limekusumbua miaka mingi au umeliomba kwa miaka mingi, utaelewa kwamba kumbe huwa kuna kufurahi mpaka unageuka kuwa kituko kwa watu wengine.
Maana unaweza kukaa ukaona fulani naye nini, mbona anatupigia kelele, mbona kila saa anaongelea jambo lile lile kwa kila mtu, hujajua amepita kwenye mazingira gani kipindi ambacho wewe ulikuwa hujui maumivu anapitia. Hata kama ulikuwa unamwona kila siku, huwezi kujua mzigo aliokuwa nao ndani ya moyo wake, maana hukuwahi kukaa naye akueleze.
Inapofika saa ya Bwana kwa mtu, akatendewa hitaji la moyo wake, furaha yake isiwe kikwazo kwako, mwache amtukuze Yesu wake. Hujui mikesha ya usiku aliyokuwa anakesha kwa tatizo alilokuwa nalo, hujui matusi ya mawifi na wakwe zake, waliyokuwa wanamtukana kwa ajili ya kukosa mtoto.
Na wewe Mungu akikutendea jambo, piga kelele za shukrani kwake, mshangilie Bwana, ruka ruka uwezavyo, maana Bwana ametenda kwako. Acha watu wakereke kwa ajili ya furaha yako, lakini fahamu wakati unateseka, hakuna aliyekuja kukusaidia kubeba mateso hayo.
Usiache kujiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa kwenye kundi hilo.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
+255759808081
www.chapeotz.com