Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, habari za kushinda ndugu, hongera kwa ushindi wa siku ya leo. Miongoni mwa waliochaguliwa kufikia muda huu, wewe ni miongoni mwao, hupaswi kuwa mnyonge, bali unapaswa kuwa na moyo uliochangamka.

Mahusiano yetu ya karibu yanaweza kutusababisha tukashindwa kabisa kumpendeza Mungu kwa kuzuiliwa na ukuta wa undugu. Lakini tumesahau aliyetuumba ndiye anaweza kutupa kibali cha kuendelea kuwa pamoja ama kumwondoa mmoja wetu.

Unakuta mtu anakosea kabisa, kwa kuwa aliyeshikilia mamlaka ni ndugu yake, anaona haina shida. Lakini kumbe anaendelea kutenda yasiyofaa na baadaye inageuka adhabu ya wote kwa Mungu.

Ikiwa mmepatana kwa jambo lolote, alafu kati yenu akaanza kwenda kinyume, usimwangalie usoni yeye kama yeye. Angalia madhara ya matokeo ya yale anayoyatenda, ni makubwa kiasi gani.

Usipoelewa matokeo ya yale aliyoyatenda na anayoendelea kuyatenda, utasababisha matatizo mabaya zaidi kwa wengine ambao hawakustahili adhabu ile.

Unaona watoto wako wanatenda mabaya, unaogopa kuwaambia kwa sababu ni wako, lakini wengine wakitenda kosa unakuwa mkali na unachukua jukum la kuwakemea na kuwachapa kabisa.
Hapo unakosea kwa sababu hakuna ulichosaidia maana kilicho miguuni mwako bado hujakiondoa, lakini unahangaika na vya pembeni.

Vyema ukaeleweka unatoa adhabu kwa yeyote yule atakayekosea, na kama unamwonya ijulikane ameonywa na wote wameona. Sio watoto wengine wanapata fimbo wakikosa na wengine hawapati fimbo na wamekosea, kwa sababu zako binafsi. Sasa unasababisha watoto wengine waone baba ana upendeleo.

Lakini hapa tunajifunza kwa mfalme Asa alivyoona mama yake mzazi anaabudu miungu mingine iliyo kinyume na Mungu wao. Alimwondoa kwenye umalikia na kuvunjavunja ile sanamu.

Rejea: Hata na Maaka mamaye Asa, mfalme akamwondolea daraja yake asiwe malkia, kwa kuwa amefanya sanamu ya kuchukiza kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake, akaiponda, akaiteketeza penye kijito cha Kidroni. 2 NYA. 15:16 SUV.

Umeona hapo ndugu, usifikiri haya nimetoa wapi, nimetoa ndani ya biblia ambayo hata wewe unayo. Ni maandiko yanayotuweka wazi kabisa kuwa anayeenda kinyume na Mungu, lazima apewe adhabu iliyowekwa.

Shida inakuja kwa baadhi ya watu makanisani, wale wenye uwezo wa chini kifedha wakikosea wanatengwa ushirika na kutangazwa kabisa mbele ya madhabahu. Na wale wengine wenye uwezo wa juu kifedha wao wakitenda kosa mambo yao yanamalizika kwa chinichini.

Lakini tunaona mfalme Asa alikuwa jasiri sana kumtoa mama yake kwenye kiti cha umalkia, kwa kosa la kuwagombanisha na Mungu wao, kwa kuabudu sanamu.

Naelewa hili jambo linahitaji ujasiri mkubwa, ila heshimu mapatano yenu mliyojiwekea, kuwa atakayeenda kinyume na taratibu zilizowekwa itabidi ashughulikiwe. Ili mwingine akiona ajue kuwa hakuna utani katika lile.

Rejea: Wakafanya agano, ya kuwa watamtafuta BWANA, Mungu wa baba zao, kwa mioyo yao yote, na kwa roho zao zote; na ya kwamba ye yote asiyemtafuta BWANA, Mungu wa Israeli, atauawa, akiwa mdogo au mkubwa, kwamba ni mwanamume au mwanamke. 2 NYA. 15:12‭-‬13 SUV.

Heshimu agano, heshimu makubaliano yenu mliyojiwekea kwa ajili ya utukufu wa Mungu, haijalishi nani atakosea. Lazima ashughulikiwe haraka ili kuokoa roho za wengine, ili wanapotazama wengine adhabu unayotoa, wajue hakuna upendeleo.

Asa alimshusha mama yake cheo kwa kosa ambalo angeweza kufumba macho ili kulinda heshima ya mzazi wake. Ila mfalme Asa hakuzuiliwa na upendo wa mama, alitazama kusudi la Mungu na kulitenda ipasavyo.

Uwe tayari kulinda wokovu wako na usikubali ndugu yako kukutoa kwenye uwepo wa Mungu, kwa sababu unampenda na hutaki mahusiano yenu yaharibike.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com