Hata kama mtu atakuwa na mabaya yake mengi anayoyafanya, yapo mazuri yake atakuwa nayo. Ndivyo ilivyo na ndivyo tulivyozoea katika maisha yetu ya kila siku.

Pia tunaamini kwamba, kama mtu amewahi kutenda mema/mazuri, siku akitenda mabaya hatupaswi kumsema vibaya, hatupaswi kumtenga kwa mabaya yake. Maana kuna wakati aliwahi kutenda mema, kuna wakati aliwahi kujitoa sana kwa mambo ya Mungu.

Wakati mwingine tunapoona watu wanawatenga wale watenda dhambi/maovu, tunawaona wanafanya isivyo sawa. Tunaona wale watenda mabaya hawakupaswa kutendewa hivyo kutokana na mema yao waliyowahi kuyatenda huko nyuma.

Wakati mwingine tumefika mahali tunaona wanaochukua jukumu hilo la kuwatenga ambao ni watumishi wa Mungu. Hawatendi ilivyo sawa, tunafikiri wangeachwa hivyo bila kutengwa kutokana na mema/mazuri yao waliyowahi kuyatenda.

Pamoja na mitazamo yetu ya kibinadamu, mbele za Mungu ni tofauti kabisa, leo unaweza ukawa vizuri Mbele za Mungu, ukawa mcha Mungu mzuri, ukawa mwaminifu mbele za Mungu. Siku ukiachana na hayo, ukaanza kumtenda Mungu dhambi, uwe na uhakika Mungu hataangalia mazuri yako ya nyuma.

Kama zamani uliishi maisha ya kumpendeza Mungu, ulijitenga na dhambi, ulijiweka mbali na maovu ya dunia hii. Siku ukiacha kujilinda na kuanza kumtenda Mungu dhambi, hukumu ya Mungu haitakuacha salama.

Kwa kufikiri/kuwaza kwako unatenda mema mengi, alafu nyuma ya pazia ni mtenda maovu aliyebobea. Uwe na uhakika usipoacha na kutubu huo uovu, uwe na uhakika uhukumu ya Mungu ikija itakuhusu. Hata kama kuna mambo mazuri unayafanya au uliwahi kuyafanya huko nyuma.

Mungu anachoangalia ni mwisho mwema na sio mwanzo mzuri, yaani kama ulianza wokovu vizuri. Alafu ukafika mahali ukaona uachane na mambo ya wokovu, ukaanza kumtenda Mungu dhambi. Huo ndio unaitwa mwisho mbaya kama hutoacha dhambi na kutubu.

Haijalishi ulitumika sana mbele za Mungu, kama utarudi nyuma na kuanza kutenda yaliyo maovu. Mungu hataangalia jinsi ulivyotumika sana mbele zake, siku ikifika ya hukumu ukiwa bado hujatubu, hukumu yake itakuhusu.

Rejea: Bali mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilolikosa, naam, katika dhambi yake aliyoitenda, atakufa. EZE. 18:24 SUV.

Hakikisha unalinda utakatifu wako, maisha yako ya wokovu yawe salama wakati wote. Usije ukafika mahali ukaona umetenda mema mengi sana ngoja ugeuke na kuanza kutenda mabaya. Utakuwa unajipoteza mwenyewe.

Tena Mungu anasema hivi; Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. Waebrania 10 :38.

Ndugu yangu, kama umepata Neema ya kumjua Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako. Hakikisha unailinda imani yako kama Lulu, usije ukaikosa mbingu kwa uzembe wako.

Tunza maisha yako ya wokovu kwa gharama yeyote ile, ili usije ukaikosa mbingu kwa vitu ambavyo ungeweza kuviepuka.

Mungu atusaidie sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081