
Ndugu yangu, hii ni fursa kwetu wote waaminio, bila kujalisha mazingira uliyozaliwa nayo, bila kujalisha shule uliyosoma, bila kujalisha historia yako mbaya ya nyuma, bila kujalisha una pesa nyingi, bila kujalisha huna fedha hata shilingi moja mfukoni mwako.
Fahamu kwamba Mungu hana upendeleo, hata kama ulikuwa unawaza kuwa Mungu ana upendeleo, kuanzia sasa hivi anza kufanya mazoezi ya kuondoa huo mtazamo wako hasi. Naimani hadi kumaliza kusoma makala hii, utakuwa umepata kitu cha kukusaidia katika maisha yako.
Mungu haangalii usoni kama wanadamu wanavyoangalia, watu wanaweza kuangalia uzuri wa sura yako wakakupa kazi kutokana na mwenekano wako mzuri. Lakini mbele za Mungu ni tofauti kabisa, usafi wa moyo wako ndio unatakiwa mbele za Mungu, haijalishi hukumbuki mara ya mwisho kununua nguo mpya ni lini, hilo suala ni lingine kabisa ila sio hoja ya msingi ya kukufanya ufikirie hivyo.
Huwa tunafika mahali tunaanza kuona Mungu ana upendeleo, hasa tunapoona wengine wanazidi kustawi huku sisi tukipita katika nyakati ngumu. Hasa pale tunapoona wengine wanapata watoto wazuri, lakini sisi tumehangaika miaka ya kutosha bila ya kupata hata mtoto mmoja.
Huwa tunaona Mungu ana upendeleo pale tunapofika hatua tunaona wengine wamemaliza shule/chuo muda sio mrefu sana, lakini wanafikia kupata kazi nzuri huku sisi tukisota mtaani miaka ya kutosha bila kupata kazi. Kama ni maofisi tumezunguka sana na bahasha zetu, kama ni maombi ya kazi tumeomba sana online, lakini hatujaambulia chochote.
Umefika hatua ya kuamini Mungu ana upendeleo, hasa pale ulipowaona rafiki zako ambao ulikuwa nao, wao wameolewa wote ila wewe hadi sasa unaishia kuumizwa kwenye mahusiano kwa kuachwa na kila mwanaume anayekuja kwako.
Ukiangalia umri ulionao na maneno unayosikia juu yako hadi wakati mwingine unafika hatua unajisikia kama kuzimia moyo, maana unaona kama giza mbele yako. Wakati mwingine unafika hatua unasema bora ukae hivyo hivyo bila kuolewa, ukikaa baada ya muda fulani unasikia tena msukumo wa kuolewa na wa kukuoa humwoni.
Umefika hatua unaona Mungu ana upendeleo pale unapoona vijana wadogo wamekukuta kazini una miaka mingi, una elimu ya kutosha, una uzoefu wa kutosha. Lakini wao wanapandishwa cheo, wewe upo cheo kile kile, na wala huoni dalili zozote za kupandishwa cheo.
Umefika hatua unaona Mungu ana upendeleo, kwa jinsi ulivyopambana na maisha, umejaribu kila njia kuhakikisha unapata fedha, lakini pamoja na hayo mapambano hadi leo hujafikia lengo. Lakini unaona wengine wanazidi kufanikiwa kwenye biashara zao, wanazidi kujenga majumba makubwa na mazuri, wewe hata nyumba ya kuishi na watoto wako imekushinda.
Ukiangalia hayo yote niliyokutajia na mengine ambayo sijafanikiwa kukutajia kutokana na ufinyu wa nafasi yangu, unaweza kufikiri Mungu ana upendeleo sana kwa baadhi ya watu. Na unaweza kufika mbali zaidi kwa kufikiri kuna watu wamezaliwa na bahati zao, na wengine wamezaliwa hawana kabisa bahati hizo.
Mawazo hayo yote ni kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu, Mungu wetu hana upendeleo kwa mtu yeyote, haijalishi unaonaje kwako ila fahamu hili jambo kuwa Mungu wetu hana upendeleo wa aina yeyote ile.
Rejea: Kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu. RUM. 2:11 SUV.
Ndugu yangu, kama ulikuwa unajisemea moyoni mwako kuwa Mungu ana upendeleo sana, kuanzia sasa futa hilo wazo. Kwanini nakuambia hivyo, kwa sababu napata uhakika kutokana na maandiko matakatifu, haya ndio yananipa ujasiri wa kukuambia Mungu hana upendeleo.
Ukimcha Mungu na kumtumikia kwa moyo wako wote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote, Mungu atakuinua zaidi ya wengine, Mungu atakuketisha na wakuu, bila kujalisha historia yako ya nyuma, na bila kujalisha ulizaliwa kwenye familia ya kimaskini sana.
Bila kujalisha uliokotwa jalalani na wasamaria wema ukiwa katoto kachanga baada ya mama yako kukutupa, na huyo mama humjui hadi sasa, wala baba yako humjui na hujawahi kumwona. Jina lako na la mzazi unalolitumia umepewa na yule aliyekuokota na kukulea.
Fahamu kwamba Mungu hana upendeleo, wala huwezi kumpa/kupewa rushwa, wala wale unaowaona wamefanikiwa zaidi hakuna rushwa waliyotoa kwa Mungu. Usidanganywe kabisa, utakuwa unakwama mahali kwa sababu ya kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu kama utakuwa umeokoka sawasawa.
Rejea: Kwa maana BWANA, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa. KUM. 10:17 SUV.
Sijui kama umesoma hilo andiko vizuri na ukalielewa, hebu rudia tena kusoma hilo andiko nililokupa hapo, utaona limeeleza jambo kubwa sana la kukusaidia katika kipindi ambacho unaona Mungu ana upendeleo kwa baadhi ya watu.
Mungu wetu ni wa haki, ukiwa mwaminifu kwake hataakuacha, yaani namaanisha kwamba umeokoka vizuri Yesu Kristo ni Bwana na mwokozi wa maisha yako, Neno la Mungu lipo la kutosha moyoni mwako, unajitoa kwa mambo ya Mungu. Nakuambia Mungu hana upendeleo atakuinua zaidi ya hapo ulipo sasa, lile unamwomba sana atakupa tu kwa wakati wake.
Rejea: Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. MDO 10:34-35 SUV.
Nami naungana na mtumishi wa Mungu Petro, anasema ametambua Mungu hana upendeleo, bali ni Mungu wa haki. Ukimcha Mungu kwa uaminifu atakupa haja ya moyo wako sawasawa na mapenzi yake, ukiwa unamtumaini Mungu hutoabika kamwe, nakuhakikishia hili ndugu yangu katika Kristo unayesoma ujumbe huu.
Na kama hujaokoka na unasoma ujumbe huu, nakushauri umepokee sasa Yesu Kristo awe Bwana na mwokozi wa maisha yako, Yesu huyu ninayemsema hapa habari zake ndiye aliyenifanya mimi niweze kukueleza haya leo. Wanaonifahamu wanaweza kukubaliana na mimi, na wewe huna haja sana kuhangaika kunifahamu kama wengine ila niamini ninachokuambia hapa kupitia maandiko matakatifu niliyokupitisha.
Mungu ninayemtumikia mimi na ninayesema habari zake hapa ni halisi, ndiye huyu huyu ninayekueleza habari zake hapa za kutokuwa na upendeleo wa aina yeyote kwa mtu, wala sio Mungu wa kuweza kupewa rushwa na mtu wa aina yeyote.
Mwisho, kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa kwenye kundi.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com