Kuisema kweli ya Mungu, kuihubiri injili isiyogushiwa, kukemea dhambi bila kuangalia mtu usoni kwa nafasi aliyonayo kwako au kwa jamii, kuisema kweli bila kujalisha watu watakuchukuliaje, kutamka waziwazi au kumkiri Yesu Kristo mbele za watu kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, si jambo linalowezwa kutamkwa na kila mkristo.

Wengi wanakiri kuwa wameokoka sawa ila hawana ujasiri wa kutamka kuokoka kwao kwa watu wengine, hata matendo yao wakati mwingine yanapingana na kuokoka kwao. Ndio maana wanapofika mahali ambapo wanapaswa kuonyesha wao ni watu wa namna gani huwa wanakwepa.

Ujasiri wa kukemea dhambi kwa wakristo wengi, au kwa watumishi wengi, huwa ni jambo linaloonekana gumu kidogo kwao. Hii inaweza kutokana na kuogopa kuvuruga uhusiano wake na mtu ambaye alikuwa anamsaidia mambo mengi.

Wengine hawana ujasiri wa kuwaambia marafiki zao kweli ya Mungu, hata pale wanapotakiwa kuonyesha misimamo yao mbele za Mungu. Misimamo hiyo huwa inakosekana kabisa kutokana na kuonea haya kile wanacho ndani ya mioyo yao.

Mtu anaweza kuulizwa mbele za watu, umeokoka? Anaweza kukataa waziwazi au anaweza kumuuliza uliniona wapi kuwa mimi nimeokoka? Anaweza kukataa ukristo wake kwa sababu ambazo hazina msingi mbele za Mungu.

Kukataa kwetu au kumwonea haya Yesu Kristo mbele za watu, hili haliwezi kutuweka kwenye nafasi nzuri sana, hii inatuweka kwenye nafasi mbaya sana. Ninaposema mbaya namaanisha kweli kweli, maana inashiria siku ya mwisho na Baba yetu aliye mbinguni atatukataa kabisa.

Huwezi kumkana Yesu Kristo mbele za watu ukabaki salama, huwezi kumwonea haya Yesu Kristo mbele za watu ukabaki salama. Hili tunajifunza ndani ya biblia takatifu;

Rejea: Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu. MK. 8:38 SUV.

Unawaona watu wanatenda dhambi, unawaonea haya au unaogopa kuwaambia ili usije ukaonekana mbaya. Uwe na uhakika kuogopa kwako kutakufanya utupwe kwenye ziwa la moto milele.

Ukubali ukatae, kama unaonea haya injili, hutaki kuonekana ukiisema kweli ya Mungu aliye hai. Unaona utatengwa na watu, unaona utaeleweka vibaya, unaona utatengwa na marafiki/ndugu zako. Uwe na uhakika hutaingia mbinguni, ndio hutaingia katika maisha ya furaha ya umilele.

Unaweza kusema kuona haya tu ndio inifanye nisiingie mbinguni, Yesu mwenyewe si anajua nina aibu nyingi mbele za watu. Hiyo sio sababu ya kuweza kujitetea mbele za Mungu.

Kama unamkana Yesu Kristo mbele za watu, labda kwa kuogopa kuwaambia watu acheni uzinzi, uasherati, ulevi, wizi, na mengine mengi mabaya. Usitegemee utaenda kukubaliwa na Mungu wetu, utaenda kukataliwa na Yesu Kristo mbele za Baba yake.

Rejea: Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Mathayo 10 :33.

Tafakari au jihoji mwenyewe, umemkataa Yesu Kristo mbele za watu mara ngapi? Je, umemwonea haya Yesu Kristo mbele za watu watu mara ngapi? Huenda usikumbuke kwa haraka ila unapaswa kuacha hiyo tabia kama ulikuwa nayo.

Usikubali kuikosa mbingu kwa sababu ambazo tayari Neno la Mungu lilikutahadhirisha mapema, kataa kabisa kutawaliwa na hofu zenye kukuzuia usiiseme kweli ya Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com