Changamoto kwenye hili wengi huwa hawajioni kama wamefumbwa macho yao ya kiroho.

Kama mtu hajui kama macho  yake yamefumbwa, itakuwa ngumu kutambua mahali alipo sio sahihi.

Pia atakuwa hawezi kutambua mahali alipo ni sahihi/salama, badala yake atakuwa anajiona hayupo sehemu sahihi/salama kwa sababu haoni.

Kufumbwa macho kwa mtu ni jambo ambalo lipo, sio jambo la kufikiri labda ni hadithi za kutengeneza.

Mnaweza mkawa mnasoma biblia, wapo watakuwa wanafunuliwa maandiko yale wanayosoma kwa namna ya tofauti kabisa. Na wapo watakuwa hawaoni kitu kwenye yale maandiko ambayo watu waliona cha kuwasaidia.

Macho yetu yanapaswa kuona sawa sawa na makusudi ya Mungu.

Bila kufumbuliwa macho yetu, nyakati tulizonazo tunaweza kujikuta tupo kwenye hofu kubwa kwenye mambo ambayo tungekuwa tunaona vile Mungu yupo pamoja nasi, tusingeweza kuwa na wasiwasi/hofu.

Uzuri ni kwamba kuna nafasi ya kumwendea Mungu akupe kuona, inawezekana kabisa unajiona kipofu wa kiroho. Una nafasi ya kwenda mbele za Mungu kumwomba akupe kuona.

Rejea: Elisha akaomba, akasema, Ee BWANA, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. BWANA akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote. 2 FAL. 6:17 SUV.

Ikiwa mtumishi wa Mungu Elisha aliomba Mungu na yule mtumishi akafumbuliwa macho yake. Je wewe ukiomba si itawezekana? Ndio itawezekana kabisa usiwe na mashaka juu ya hilo.

Muhimu sana macho yako ya  rohoni yakatiwa nuru, itakusaidia sana katika maisha yako ya wokovu. Yapo mambo mengi sana yanahitaji uwe umefumbuliwa macho yako ndio uweze kuyashinda au kuyafanya.

Hili tunaliona kwa mtumishi wake Elisha, alijawa na wasiwasi mwingi na kushindwa afanye nini. Lakini  mtumishi wa Mungu Elisha alimwona haoni ulinzi uliowazunguka, hakumwacha katika hali hiyo, alimwombea kwa Mungu akafumbuliwa macho yake.

Nawe kama huoni na umejawa na wasiwasi mwingi juu ya hatari iliyo mbele yako. Ombi langu kwa Mungu afumbue macho yako uweze kuona ulinzi wa Mungu ulivyo mkubwa juu yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
+255759808081