Moja ya eneo ambalo linawapa changamoto wengi ni pale mtu anapofika muda wa kuhitaji kuoa/kuolewa ila anakuwa haoni yule anayemhitaji, wengine uvumilivu huwashinda na kujikuta wanaingia kwenye mahusiano ambayo hawakuyataka au hawakuyatarajia.
Kuchelewa kuoa/kuolewa kunachangiwa na sababu mbalimbali, mwenye changamoto hii asimpomtegemea Mungu, au Imani yake ikiyumba, au asipopata washauri wazuri, atafanya maamuzi ambayo sio sawa. Anaweza akawa mtu wa huzuni kila mara kwa sababu ya kuchelewa kuoa/kuolewa.
Unaweza kushinda hii hali ngumu na ukafikia hatima njema, yaani ukaoa/ukaolewa na mtu sahihi kwako na ukafurahia maisha yako ya ndoa katika umri wako uliobaki hapa duniani.
Hebu tuone hatua hizi 5 za kukusaidia unapojikuta umri umeenda na unahitaji kuoa/kuolewa ila huoni wa kukuoa, au kila anayekuja kwako anakuacha, au kila unayemchumbia uchumba wenu haufikii hatima njema, nikiwa na maana hamfiki mwisho.
1. Mwamini Mungu.
Hili la kumwamini Mungu linaweza lisiwe jambo la msingi tena kwa wengi baada ya kusubiri kwa muda mrefu, lakini ni silaha muhimu sana kwa mwamini yeyote mwenye safari ya kwenda mbinguni.
Tunapaswa kuendelea kumwamini Mungu hata unapojiona tumechelewa, kumwamini Mungu kunakusaidia kuendelea kumwomba akusaidie haja ya moyo wako. Ukiondoa tumaini mbele za Mungu ni rahisi kufanya maamuzi yasiyo sahihi kwako.
Usitishwe na marafiki, ndugu, wazazi, kwa kuambiwa kuwa uzae tu na yeyote kwa dhana kwamba “usije ukafa bila kuacha uzao wako” hii ni dhana inayotumika sana na inawafanya wengi kujidumbukiza kwenye mahusiano yasiyo sahihi na yanayozaa majuto kwao.
Mwamini Mungu, usikumbuke makosa ya nyuma, ikiwa umeokoka na umejiweka sawasawa kwa Yesu, uwe na uhakika Mungu atakupa haja ya moyo wako. Utamfurahia Mungu kwa kukupa haja ya moyo wako, kwa kumwamini na kuvumilia katika kipindi chote hadi akakupa mtu sahihi kwako.
2. Usijiingize Kwenye Maisha Ya Kumkosea Mungu.
Kuchelewa kuoa/kuolewa kusikuingize kwenye mahusiano ya mapenzi(uasherati), unaweza kuona ni jambo jema, ila unapaswa kuelewa sio jambo jema, linakuondolea uhusiano wako mzuri na Mungu.
Ukiwa kwenye michanganyo hutakuwa na ujasiri mbele za Mungu, alafu wakati huo huo unataka Mungu akupe mke/mume sahihi wa kuishi na wewe, mume/mke atakayekuwa baraka katika maisha yako ya ndoa.
Maisha matakatifu yanaweza kuonekana kama ni ushamba kwa yule anayejiepusha na vitendo vya uasherati, ila ushindi wa mtu anayetunza maisha yake ni mkubwa sana kuliko yule anayechanganya mambo.
Maisha ya michanganyo yanasababisha kuwakimbiza wale wanaokuja kwetu wanatukuta tupo kwenye mahusiano ya kingono na watu wengine wasio na mpango wa kuishi nasi katika ndoa.
Uwe makini, epuka kuwa chombo cha kutumia au kutumiwa na kuachwa hapo, vumilia kwa muda mchache ili Mungu akupe au akukutanishe na mtu sahihi. Unaweza kujiuliza utamjuaje mtu sahihi au Mungu atakupaje, ukiwa umetulia na ukiwa na uhusiano mzuri na Mungu, ni rahisi kutambua hilo.
3. Usijidharau/Usijikinai.
Hili sio ajabu kulikuta kwa baadhi ya watu, wapo wameshajikatia tamaa kabisa ila ndani yao bado wanahitaji kuoa/kuolewa, hili linaweza kuwakumba Zaidi mabinti/wanawake. Hii hali imesababisha baadhi kuamua kufanya maamuzi ambayo yalisababisha majuto kwao.
Unapochelewa kumpata mwenzi wako wa maisha, hupaswi kujidharau kwa kujiona wewe ni duni, au wewe hufai, kujiona hivyo unajiletea hali ya kujikinai/kujidharau. Jione wewe ni wa maana sana mbele za Mungu, kujiona hivyo inakupa nguvu ya kujipenda na kujitunza.
Unapojidharau elewa kwamba anapokuja au unapokutana na mtu sahihi kwako unaweza ukamwona kwa picha tofauti isiyokuvutia kwako, anapokueleza mambo ya msingi utamwona anatania na wewe haupo hivyo kama anavyokueleza.
Eneo hili la kujidharau/kujikinai unaweza kuliona ni la kawaida ila linaweza kutumika kukukwamisha usioe/usiolewe na mtu sahihi kwako, kama ni hivyo kwanini uruhusu hali ya kujidharau? Usiruhusu hilo, hata kama umechelewa, usijikinai, Yesu bado anakuwazia mema.
4. Jikubali.
Kuna watu pamoja na kuachana na maisha ya dhambi, maisha yaliyokuwa yanamkosea Mungu, bado wanahukumiwa ndani yao, wanapohukumiwa ndani yao, hali ya kutojikubali inakuwa inawakabili ndani yao.
Wapo wengine kutokana na hali ya nyumbani kwao au kutokana na hali duni za kiuchumi, wanakuwa hawana ujasiri kabisa, kule kujikubali na kujiona na wao wanastahili kuitwa mume/mke wanaona hawafai.
Wengine wanajiona wabaya, hiyo hali imewakumbuka na wengine wanaanza kutumia madawa makali ya kujibadilisha sura zao, wengine wanajibadilisha maumbo yao ya mwili. Hii yote ni kwa sababu ya kutojikubali walivyo, na mwisho wake wamejisababishia madhara kwenye miili yao.
Usijikatae kama Mungu hajakukataa, jikubali ulivyo, kuna mahali ulikosea na ukatubu mbele za Mungu? Usiendelee kukaa na unyonge ndani yako, ishi ukijua wewe ni mtoto wa Mungu uliyesamehewa dhambi zako.
Ukiwa mtoto wa Kifalme/kikuhani, hupaswi kuishi kinyonge, hupaswi kujichukulia duni, wewe ni mtu wa maana sana, kujiona hivyo itamvutia yule mtu sahihi aliyekusudiwa na Mungu uishe naye.
Wapo watu wanawafukuza waume/wake kwa kutojikubali kwao, kwa sababu mtu asiyekubali hawezi kuwa bora kwa kitu anafanya, hata maisha yake hayawezi kuwa bora kwa sababu amejifunga katika eneo la kutojikubali.
5. Jipambambanue Kwa Mambo Ya Mungu.
Moja ya eneo nyeti sana na wengi hawajui au wengine wanalipuuza na kulichukulia kawaida ni hili la kujipambambanua, ninaposema kujipambanua ni kujiweka wazi wewe ni mtu wa namna gani.
Ninaposema hivi kuna watu hawaeleweki wameokoka au ni wapagani, utakuta mguu mmoja upo kwenye mambo yanayomchukiza Mungu, na mguu mwingine upo kwenye mambo yanayompendeza Mungu.
Mtu wa namna hii atapishana sana na wale walioamua kuingia wazima wazima kwenye wokovu, kwa sababu mambo ya kiroho huwa hayapendi kuchanganywa, maana Mungu mwenyewe hapendi michanganyo.
Kama kweli umeamua kuwa mfuasi wa Yesu, jiweke wazi kabisa, acha kona kona, hizo kona kona zitakuzalishia mapooza, alafu utaanza kulia na kusema una mikosi, mikosi unaitegeneza mwenyewe.
Ukijitunza na ukamsikiliza Mungu vizuri, uwe na uhakika utakutana na mtu wako sahihi, hajalishi umri umeenda, ukiwa na haja ya kuoa/kuolewa utapata haja ya moyo wako na utafurahia maisha ya ndoa kwa muda wako uliobaki duniani.
Mwisho, hayo ni mambo muhimu ya kukusaidia kushinda vita vya akilini mwako, ukielewa haya na kuyaishi utakuwa mtu mzuri na utawasaidia wengi sana waliopatwa na changamoto kama yako.
Tukutane wakati mwingine kwenye Makala nyingine zuri inayohusu mahusiano, ninaamini hutabaki kama ulivyo ikiwa utajifunza, na kuyaweka moyoni mwako, na kwenye matendo haya unayojifunza.
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081