Hali kama hii huwapata baadhi ya vijana, anaweza kuwa kijana wa kike au wakiume, kijana wa kiume anaweza kumpenda msichana na akatamani awe mke wake ila akakataliwa. Na binti anaweza kumpenda kijana wa kiume na kutamani awe mume wake ila jambo hilo likawa gumu kwake.
Ikiwa vijana wengi wanakutana na changamoto hii na wakati mwingine huwa wanakosa washauri wazuri na kujikuta wanaingia katika mambo mabaya pasipo kupenda wao. Ama anaweza kubaki kuhangaika bila kujua cha kufanya, na anapoona mwenzake ametangaza uchumba na mtu mwingine anabaki na chuki moyoni kwa huyo msichana/mvulana.
Tena wengine huwachukia mabinti au vijana wa kiume wanapotangaza uchumba, kwa sababu walikuwa wanataka wao waolewe au waoe huyo aliyeingia kwenye mahusiano ya uchumba na mtu mwingine.
Huenda hata hao wanaowachukia hawajui, na kama wanajua wanajitetea kuwa hawakuwahi kuongea mambo ya mahusiano zaidi kuwa marafiki tu wa kawaida kama dada na kaka.
Sasa kwa kuwa jambo hili linawasumbua wengi, hapa tunaenda kujifunza njia nzuri ya kutusaidia pasipo kumkosea Mungu wetu na kubaki tukiwa salama na amani ya mioyo yetu, bila kuathirika unapoona mambo yameenda ndivyo sivyo.
Zifuatazo ni hatua chache muhimu za kufahamu unapompenda msichana/mvulana ila yeye haonyeshi dalili yeyote ya kukupenda wewe;
1. Omba Mungu.
Hii ni hatua muhimu sana kwako kijana, kama unasikia ndani yako kuwa na amani na msichana/mvulana fulani, alafu ukajaribu kuwa karibu naye na kumweleza kile unakiona ndani ya moyo wako. Alafu akawa hakuelewi kabisa, unapaswa kwenda mbele za Mungu, muulize Mungu huyo ndiye au umesukumwa na tamaa zako za kimwili.
Ninapozungumza tamaa za mwili simaanishi tu uasherati, unaweza kuvutiwa na sura yake, unaweza kuvutiwa na kazi yake, unaweza kuvutiwa na biashara zake, unaweza kuvutiwa na elimu yake na mengine mengi. Lakini ikawa sio kusudi la Mungu la wewe kuishi na huyo, japo moyoni unaona ni mwenyewe kabisa na angefaa kuwa mume/mke wako.
Unapoenda mbele za Mungu kumwambia hitaji lako, ukiwa msikivu na ukiwa na neno la Mungu ndani yako, uwe na uhakika Mungu atakujibu ombi lako na utajua umependa sehemu sahihi au tamaa zako tu. Utakapojua hutakuwa na maswali mengine wala hutalazimisha mambo yaende kama unavyotaka wewe maana unakuwa na uhakika na yale majibu ya maombi yako.
2. Usijirahishe kwake.
Kosa ambalo wengi hufanya hasa kwa mabinti hujirahisha kwa wanaume, anaamini kuwa atakapolala naye kimapenzi atakuwa amemvuta na kumpenda yeye, bila kujua kuwa upendo huletwi na kufanya uasherati.
Vijana wengine wa kiume hufikiri akilala na binti ndio atamkubali na kumpenda, anafanya hivyo ila bado akawa anapita katika changamoto ileile, tena anaweza kumkuta ana mahusiano na mtu mwingine kabisa.
Unapompenda binti au kijana wa kiume, usiwe na hofu wala mtu asikudanganye ufanye mambo yanayomkosea Mungu wako, uwe na subira, endelea kumwomba Mungu na kusubiri.
Ikiwa ni wa kwako, uwe na uhakika atakubali na mtakuwa mwili mmoja kwa kufunga ndoa naye, ukiharakisha mambo na kutaka yaende haraka kama unavyotaka. Unaweza kuingia kwenye eneo ambalo sio la kwako na ukaja kuanza kupata shida wakati ulikuwa na nafasi ya kutokuingia huko.
3. Nenda kwa mchungaji wake/wako.
Hichi ni kitendo cha kijasiri sana, umeona umepitia hatua zote za msingi na kuona bado hakuelewi, vizuri kwenda kwa mchungaji wake ikiwa hamsali naye, na kama mnasali naye nenda kwa mchungaji wenu.
Usiwe na aibu, mweleze hitaji lako na unataka akusaidie nini, uwe wazi kabisa na ikibidi mweleze hatua ulizopitia na bado hakuelewi. Wachungaji wanajua vizuri cha kufanya, watakusaidia na utatoka ukiwa salama, ikiwa ni jambo la Kimungu ufanikiwa kuolewa naye au kumuoa.
Hizo ndio hatua chache zinazoweza kukusaidia pale unapompenda mtu alafu akawa hakuelewi, ukifuata hizo hatua chache, utavuka salama bila kujiingiza kwenye mambo yasiyofaa mbele za Mungu.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
+255759808081
www.chapeotz.com