Mungu wetu ametupa mwelekeo wa maisha yetu tukiwa hapa dunia na baada ya kuondoka dunia, neno lake na watumishi wake wanafanya kazi kubwa kuwaeleza watu ukweli.

Wapo wanaoelewa na kufuata kile wanaelekezwa, na wapo ambao wanasikiliza na kupuuza kile Mungu anawaambia wafanye na wasifanye.

Wapo wengine ambao tayari wamepomkea Kristo kama Bwana na mwokozi wao, lakini wanafika mahali wanarudi nyuma. Nikiwa na maana kwamba wanaanza kumtenda Mungu dhambi.

Yapo majina ya wale ambao wanatenda mazuri, wale wanaoishi maisha matakatifu, wale wanaomtumikia Kristo katika roho na kweli. Majina yao yapo kwenye kitabu cha Mungu.

Kitabu hichi ni cha wale watu ambao wamemkubali Kristo kama Bwana na mwokozi wao, na pale wanapomkataa au wanapomwacha kwa matendo yao mabaya. Majina yao yanafutwa kwenye kitabu cha Mungu.

Musa anamwambia Mungu amfute kwenye kitabu chake kama hatawasemehe wana wa Israel, kwa kutengeneza sanamu na kuanza kuiabudu wakati yeye yupo mlimani.

Sikia jibu la Mungu alilompa Musa kuhusu ombi lake alilomwomba, utaelewa jinsi gani Mungu hufuta majina ya watu wa namna gani.

Rejea: Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika. KUT. 32:32 SUV.

Hilo ni ombi la Musa kwa Mungu, Mungu wetu ni mwaminifu sana hakunyamaza kimya. Akamwelekeza Musa watu ambao wanapaswa kufutwa kwenye kitabu na wasiopaswa kufutwa.

Rejea: BWANA akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. KUT. 32:33 SUV.

Dhambi ndio itakayoniondoa mimi kwenye kitabu cha Mungu, dhambi ndio itakayomwondoa ndugu yako kwenye kitabu cha Mungu, dhambi ndio itakayokuondoa wewe kwenye kitabu cha Mungu.

Dhambi ndio itakayomwondoa mtoto wako kwenye kitabu cha Mungu, dhambi ndio itakayomwondoa mume/mke wako kwenye kitabu cha Mungu.

Dhambi ni mbaya sana, inatufanya tuondolewe haraka kwenye kitabu cha Mungu. Ukiondolewa maana yake jehanamu inakuhusu, lile ziwa la moto litakuhusu.

Sio kana kwamba nakutisha, Mungu anamweleza wazi Musa ni akina nani hawapaswi kuondolewa kwenye kitabu cha Mungu, na akina nani wanapaswa kuondolewa kwenye kitabu cha Mungu.

Ukiwa kama mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni hupaswi kukubali kujiingiza kwenye dhambi. Maana tumeshaona madhara ya dhambi ni kutufuta kwenye kitabu cha Mungu.

Mungu atusaidie sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081