Haleluya,

Hekima ni kiungo muhimu sana kwa mkristo yeyote yule, hekima itakulinda na mambo mengi sana, hekima itakuepusha na matatizo mengi sana.

Mitengo yeyote ya mwovu shetani inaweza kuteguliwa na hekima ya kiMungu iliyojaa ndani ya mwamini.

Hekima inapaswa kuwa kwako na kwangu, tena unapaswa kumwomba sana Mungu akupe hekima kama huna. Maana pasipo hekima unaweza kujiingiza kwenye matatizo ambayo ungekuwa na hekima usingeweza kuingia.

Mtu asiye na hekima alafu akawa kiongozi, kuna asilimia kubwa sana kuwaingiza anaowaongoza kwenye matatizo. Tofauti na mwenye hekima anaweza kuwafikisha salama, hata kama kutatokea changamoto ngumu njiani.

Hekima ya Mungu ni bora zaidi kuliko hekima za kibinadamu, hekima ya kiMungu ikiwa ndani yako. Una usalama mkubwa sana, linaweza kuja jambo fulani la mtego kwako, utaweza kuunasua mtego ule kwa kutumia tu hekima na ufahamu ulio ndani yako.

Ukiwa na hekima huna haja ya kukariri mambo, pale linapotokea jambo lolote. Hekima yenyewe itakusaidia kumalizana na lililo mbele yako.

Dada unapaswa kuiambia hekima iwe kama kaka yako anayeweza kukushauri mambo mazuri ya kiMungu. Kaka unapaswa kuiambia hekima iwe kama dada yako unayemwamini na kumpenda, anayeweza kukuambia jambo lolote ukamsikiliza.

Bila kusahau busara/ufahamu uwe rafiki yako, yapo mambo utahitaji utumie busara. Pasipokuwa na busara utakuwa unafanya mambo ya kukera watu kiasi kwamba unageuka kero badala ya baraka.

Unaweza usijue kama unakosea, kutokana na jinsi ulivyolelewa kiroho. Juhudi zako za kuutafuta uso wa Mungu ndio zinaweza kumfanya mtu akawa salama.

Jiambatanishe na hekima na busara au unaweza kusema ufahamu, hivi vitu ni vya muhimu sana kwa mkristo yeyote yule. Unaweza kuwa umeokoka lakini umekosa hivi vitu vya msingi.

Leo umejifunza, hakikisha hekima ya kiMungu inakuwa kama dada yako, na hakikisha huyu bwana busara anakuwa rafiki yako wa karibu sana.

Rejea: Mwambie hekima, Wewe ndiwe umbu langu; Mwite ufahamu jamaa yako mwanamke. MIT. 7:4 SUV

Mungu akusaidie kufahamu zaidi haya niliyokueleza hapa.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
+255759808081