“Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu”, Mt 17:20 SUV.

“Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu”, Mt 17:20 SUV.

Kama kuna kitu kina nguvu katika maisha ya mwanadamu ni imani, ukiwa na imani mbele za Mungu inaweza kukupa matokeo makubwa, na ukiwa huna imani unaweza ukakosa kile unachotaka Mungu akutendee.

Wengi tunaweza kujiuliza imani nini, kwa lugha nyepesi ninaweza kukuambia imani ni kibebeo cha mahitaji yako, ukiwa na imani unapewa kile unachoomba au kuhitaji Mungu akusaidie au akutendee.

Imani inaumba kitu au jambo lisiloonekana kwa macho ya nyama, ukiwa na imani watu wanaweza kukuona mtu uliyechanganyikiwa kutokana na vile unaamini vitu ambavyo havipo.

Pamoja na kuonekana kama mtu usiye na akili sawasawa kutokana na imani yako, tunapaswa kuwa nayo hii imani, imani ambayo inaweza kukupa chochote unachohitaji mbele za Mungu.

Ukiwa na imani sahihi mbele za Mungu, kwa lugha nyepesi tunaweza kusema wewe una chombo au silaha muhimu na kubwa kuliko zote, silaha yenye uwezo wa kukusaidia shida yeyote sawasawa na neno la Mungu.

Mara kwa mara Yesu alizungumzia sana kuhusu asili ya imani ya kweli, imani zipo nyingi ila imani aliyokuwa anaizungumzia Yesu ni ile ya kweli. Alizungumzia hasa juu ya imani iwezayo kuhamisha milima.

Imani ambayo inasababisha miujiza na uponyaji, na kutimiza mambo makuu kwa ajili ya Mungu, ambayo yameahidiwa na Mungu juu ya maisha yetu, wakati mwingine tunaweza kuyakosa kutokana na kukosa imani mbele zake.

Hebu tuone ni imani ya namna gani inayozungumziwa na Yesu?

  1. Imani ya kweli ni imani itendayo kazi kwa uhalisi na ambayo huleta matokeo makubwa kwenye maisha ya mtu, ndiyo ile imani ya kuhamisha milima. Hii inaonyesha wazi nguvu ya imani ilivyo thabiti.

2. Imani ya kweli haimanishi imani juu ya imani nyingine, ukimwamini Mungu anaweza hiyo inatosha na ndiyo imani yako, huhitaji imani ya miungu mingine. Mitazamo ya watu inaweza ikawa kinyume na imani yako ila ukiwa na uhakika unachoamini hupaswi kuogopa.

“Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu”, Mk 11:22 SUV.

3. Imani ya kweli ni kazi ya Mungu ndani ya mioyo ya Wakristo  (Mk 9:24; Flp 2:13). Inayohusu ufahamu wa hali juu unaowekwa ndani ya mioyo yetu na Mungu mwenyewe, tunakuwa na uhakika kwamba maombi yetu tuliyoomba kwake yamejibiwa na yamekuwa yetu.

“Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake”, Mk 11:23 SUV.

Imani hii inaumbwa ndani yetu na Roho Mtakatifu na inakuwa halisi, hatuitengenezi kwa ujanja na ujuzi wetu wenyewe ndani ya fahamu zetu, yupo msaidizi wetu anayetusaidia kuiumba ndani yetu.

4. Imani ya kweli ni karama itolewayo kwetu na Kristo, ikiwa ni hivyo muhimu kumkaribia Yesu na Neno lake, sivyo hivyo tu! Na kuzama zaidi katika kujitoa kwetu kwake, na kumtumainia yeye siku zote za maisha yetu.

“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo”, Rum 10:17 SUV.

Ukiwa humwamini Yesu au ukiwa unamkataa Kristo, ujue hiyo siyo imani ninayoisema hapa, tunapaswa kumwamini mwanzilishi wa imani hii, ukitaka kuwa na imani thabiti unapaswa kuwa thabiti kwa Yesu Kristo.

Siri ya uimara wa imani yetu ni kumwamini Yesu sawasawa, bila kuwa na mashaka na yeye, bila kuangalia wengine wanavyombeza, Shetani anajua uwezo wa imani ya Kristo ndani yako, ili akuweze anahitaji kuiharibu imani yako kwanza. Usikubali hilo litokee kwako.

5. Imani ya kweli iko chini ya mamlaka ya Mungu na si vinginevyo. Imani inatolewa kwa msingi wa upendo wa Mungu, hekima yake, neema yake na makusudi yake ya ufalme wake.

Inatolewa ili kutimiza mapenzi yake na kuonyesha upendo wake kwetu wanadamu tunaomwamini yeye, imani hii haipaswi kutumika kwa matakwa yetu binafsi, yaani sio mali yetu au ya mtu fulani.

Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu”, Yak 4:3 SUV.

Ukiibinafisha imani yako, utaanza kuomba maombi yaliyo kinyume na neno la Mungu kwa ajili ya tamaa zako mwenyewe, na usipojibiwa utaona Mungu hasikii maombi yako. Unaweza kukasirika na kutafuta msaada kwa miungu mingine, njia ambayo ni chukizo mbele za Mungu.

Hebu ione imani kwa namna ambayo tumejifunza hapa, utamwona Mungu katika maisha yako yote, na hutakuwa mtu anayeyumbishwa na kila upepo unaokuja kwenye maisha yake. Maana utakuwa mkristo imara mwenye misingi imara katika ukristo wake.

Ili ufahamu haya unahitaji kuwa neno, nikualike kwenye kundi la wasap la kusoma neno la Mungu kila siku na kutafakari kwa pamoja, ili uwe kuunganishwa kwenye kundi hili fanya hivi; wasiliana nasi kwa wasap namba +255759808081.

Soma neno ukue kiroho

Mungu akubariki sana

Samson Ernest