Neno la Mungu linatuhimiza kuwatii wazazi wetu, hilo lipo wazi kabisa ila unapaswa kujua vitu gani vya kufanya mzazi anapokupa maagizo. Mzazi wako anaweza akawa hajaokoka, akakupa kazi ambayo ipo kinyume na Neno la Mungu, hupaswi kumkubalia kwa sababu ni mzazi wako.

Sio kwa sababu umeambiwa uwe mtiifu, uwe unatii kila jambo ambalo linakutokea mbele yako. Lazima ujue hivyo vitu vinaendana na imani yako? Unaweza ukaalikwa mahali ambapo kupo kinyume kabisa na maadili ya kiroho, usiende tu kwa sababu umealikwa na marafiki zako.

Usitii tu kila jambo kwa sababu mkubwa wako amekuambia ufanye, kama amekuambia ufanye jambo ambalo lipo kinyume na Neno la Mungu. Hupaswi kukubaliana naye, bora uonekane huna adabu lakini ukawa umeilinda imani yako.

Kumtii Mungu ni bora zaidi kuliko mwanadamu, kumsikiliza mwanadamu mwenzako na kuacha kumtii Mungu, ni kosa kubwa sana ambalo litagharimu maisha yako.

Hupaswi kumtii mtu yeyote anayekuzuia kuokoka, haijalishi ni nani yako, kama anakuzuia kuokoka, huyo hupaswi kumtii, na kufanya hivyo huna hatia mbele za Mungu.

Hupaswi kumtii mtu yeyote anayekuzuia kutangaza habari za Yesu Kristo, haijalishi ni mtu mwenye cheo kikubwa sana kwenye nchi hii. Bora kutii agizo la Yesu Kristo la kuhubiri injili kuliko kumsikiliza mwanadamu ambaye na yeye anahitaji msaada wa Mungu.

Rejea: Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. MDO 5:29 SUV.

Mtii Mungu rafiki yangu, ukimtii Mungu hakuna mtu utaweza kumdharau, hata kama watakuona huna utii, kwa sababu hujawasikiliza wanachotaka wao. Usiondoe imani yako katika kusimama katika kweli ya Mungu, bila kujalisha wangapi wanakuunga mkono na wangapi hawakuungi mkono.

Unaposoma Neno la Mungu, usisome kujifurahisha, soma kujifunza kitu kipya katika maisha yako, hakikisha unasoma Neno la Mungu na kuliweka kwenye matendo.

Usikazane kumtii mwanadamu huku unaendelea kumkosea Mungu, bora uonekane huna nidhamu ila uwe umemtii Mungu wako. Hili ni muhimu sana kuzingatia katika maisha yako ya wokovu, na katika huduma zako.

Kama unahitaji kujiunga na kundi la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya wasap, karibu sana, tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com