Tumeshazoea njaa za kukosa chakula, tena njaa kubwa sana ambazo zimefanya watu wengine kufa kabisa. Sio wanadamu tu, tumeshuhudia njaa ya kukosa malisho ya mifugo yetu.

Tumeshuhudia mifugo mingi ya wafungaji ikikosa malisho ya majani, kwa sababu ya ukame. Hili limetokea mara nyingi hasa kwa wafungaji wanaelewa sana hili.

Pia tumeona ukame wa maji, kuna kipindi shida ya maji ilikuwa kubwa sana baadhi ya mikoa. Ukame huo wa maji umekuwa ukigusa makundi yote, kundi la binadamu, kundi la wanyama, kundi la ndege, na mimea kwa ujumla.

Haya yote tumekuwa tukishuhudia kwa uwazi kabisa, hata tunaposikia sehemu fulani kuna njaa kali. Sio Neno geni kwetu, sio taarifa ngeni kwetu, ni taarifa ambazo tumezoea kuzisikia.

Pamoja na kuzoea kusikia hayo, na huenda sio kusikia tu, umewahi kulala njaa kwa kukosa chakula, umewahi kupata shida sana ya maji, na umewahi kupoteza mifugo yako kwa ajili ya njaa kali. Ipo njaa nyingine ya kiroho itakuja.

Siku yaja ambayo hutolisikia Neno la Mungu likihubiriwa, wala hutolisikia Neno la Mungu likifundishwa. Wala hutopata mtu wa kukuhimiza usome Neno la Mungu, itakuwa ni njaa kweli kweli.

Unaweza kuchukulia kawaida ila nakuhakikishia haya yote yatatokea, si njaa ya chakula, si ukame wa kukosa mvua, ni njaa ya chakula cha kiroho. Hutopata sehemu yeyote ya Neno la Mungu.

Muda unaocheza nao sasa, unajiona huna muda wa kumpa Mungu kwa ajili ya kusoma Neno lake, na kwa ajili ya kwenda kusikiliza watumishi wake wakihubiri/wakifundisha. Ipo siku yaja hutolisikia Neno la Mungu hata kwa bahati mbaya, utakuwa na kiu kweli ila hakuna mahali utakata kiu yako.

Muda ni sasa, usiseme kesho, ni sasa, unao uamzi wa kuyatafuta maneno ya Mungu sasa kwa bidii. Neno la Mungu linatuweka wazi kabisa kuhusu haya, yaja siku, siku isiyo na jina, hayo yote utayaona dhahiri.

Rejea: Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya BWANA. Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la BWANA, wasilione. AMO. 8:11‭-‬12 SUV.

Kila mmoja atatanga tanga kila mahali ila hatoliona hilo Neno la Mungu, ni kama vile jambo lisilowezekana kabisa. Amini amini nakwambia Mungu hasemi uongo.

Mambo yote yatapita ila Neno la Mungu litasimama daima, jiweke tayari, jaza vizuri kibubu chako. Uwe tayari wakati wote, na tunza sana utakatifu wako.

Mungu akubariki sana.
Imeandikwa na Samson Ernest
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081