Nafasi nyingi ambazo wengi wanazipata, iwe kazi ya kuajiriwa, liwe eneo la biashara, iwe nafasi yeyote ile ya kujipatia fedha. Mara nyingi sio kana kwamba huyo aliyeipata alistahili sana kuliko wengine.

Wengine wasiojua huwa wanaanza kujisifia/kujitapa na kujiona wao walikuwa na haki ya kuipata hiyo nafasi aliyoipata au anayoenda kuipata.

Anamwona huyo aliyekuwepo mwanzo kwenye nafasi hiyo hakustahili sana, bali yeye ndio anastahili zaidi ya mwenzake.

Anaweza kujiona hivyo kwa sababu yeye ana uwezo zaidi wa kifedha ndio maana amepewa hiyo nafasi, anaweza kujiona kwa sababu yeye ana elimu kubwa zaidi ya mwenzake ndio maana amepewa hiyo nafasi.

Anaweza akajiona yeye ana haki sana kuliko wengine, kufikiri hivyo akasahau nafasi ya Mungu aliyompa. Ama akashindwa kujua kwanini yeye apewe na wengine waondolewe kwenye nafasi hiyo.

Tunachopaswa kuelewa hapa ni kwamba zipo nafasi tunapata sio kana kwamba tuna haki sana, ni kwa sababu wale waliokuwa wamezikalia hizo nafasi walikosea mahali.

Mungu kwenda kuwapa nchi ya ahadi wana wa Israel na kuwaondoa mataifa makubwa, wana wa waanaki, ambao hawakuwa watu wadhaifu. Israel kupewa hiyo nchi ilikuwa ni kwa sababu ya uovu wa hao watu mbele za Mungu.

Rejea: Usiseme moyoni mwako, BWANA, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia BWANA niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya BWANA awafukuza nje mbele yako. Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya BWANA, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno BWANA alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. KUM. 9:4‭-‬5 SUV.

Hii inatufundisha nini? Unapaswa kuelewa vizuri sana hapa, unaweza ukapata nafasi fulani nzuri sana. Usipotambua kilichokufanya upewe hiyo nafasi unaweza usiwe na muda mrefu sana kwenye hiyo nafasi.

Hili linalenga maeneo mengi sana, sasa kama mkristo mwenye ufunuo wa neno la Mungu ambao unatokana na kusoma kwako neno, au kutokana na mafundisho ya neno la Mungu. Hupaswi kufanya kosa katika hili, unapopata nafasi usijivune na kuona wengine hawafai.

Fahamu kupata kwako nafasi hiyo ni kwa sababu ya kutumia kwao vibaya madaraka, kwa maana nyingine Neema ya Mungu ndio iliyokufanya uwe hapo ulipo.

Hapa ndipo umhimu wa kusoma neno la Mungu kila siku na kutenga muda wa kutafakari yale uliyojifunza unapokuwa na umhimu mkubwa sana kwa maisha ya mkristo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com