Nimekutana na swali hili kutoka kwa vijana, hasa mabinti wanauliza sana hili swali, na wengi wanauliza wakiwa tayari wameshaingia kwenye mahusiano. Sasa anakuwa anaona tabu kujitoa kwa mtu anayempenda alafu imani zao zipo tofauti.

Tunapozungumza imani naomba uondoe mtazamo ulionao hasa mtazamo wa dini au dhehebu, tuzungumzie imani, ninaposema imani nalenga imani katika Yesu Kristo. Jambo lingine ambalo tutagusia kidogo ni misingi ya imani yenu inaendana au ipo tofauti na upo tayari kuendana nayo?

Tunapozungumzia mahusiano ya ndoa tunazungumza eneo nyeti sana la maisha ya kijana hadi uzee au hadi kifo kiwatenganishe, kwahiyo hatupaswi kulichukulia kawaida na tukalifanya kama jambo ambalo halipaswi kupewa uzito wowote.

Kabla ya kuingia kwenye mahusiano ya uchumba au ndoa, unapaswa kujua hilo, ukishajua hilo ile hali ya kufanya maamuzi yanayosukumwa na marafiki au wazazi au mihemko yako binafsi hutafanya hivyo.

Wewe ni mkristo alafu unakutana na binti au kijana wa kiume wa kiislamu anakupenda sana, anaonyesha kukujali na ana zile sifa baadhi unazozitaka ila mnakuwa mnatofautiana imani. Yeye hamwamini Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake, wewe unakuwa unamwamini YESU.

Hili ni jambo nyeti sana kwako, ikiwa mnatofautiana katika kuamini na mnataka mkajenge ndoa iliyo imara, uwe na uhakika utakuwa umeanza kukosea msingi wa ndoa yako hata kama unaona mwenzako anakupenda sana.

Moja ya mambo muhimu kwenye ndoa yako au moja ya msingi wa ndoa yako ni imani, kama utampishana kwenye imani alafu unataka kulitimiza kusudi la Mungu katika maisha yako. Ujue utakuwa umeanza kusema sihitaji kutimiza hilo kusudi la Mungu maana utakuwa umemtafuta mpinzani wa maisha yako kwa kuwa unaye ndani kwako kwa makubaliano sahihi ya kisheria.

Biblia inasema; Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? 2 KOR. 6:14 SUV.

Ukifungiwa nira na asiyeamini sawasawa na wewe, tayari utakuwa umetengeneza tatizo la kwanza kwenye ndoa yako, pia utakuwa umeharibu msingi wa ndoa yako. Mtakuwa mnasumbuana kwenye eneo hilo na litawaletea vurugu ndani ya nyumba yenu.

Kwahiyo usiingie kwenye ndoa na mtu ambaye  tangu utoto wake hadi amekua anaambiwa mkristo ni kafiri, na wewe unamwona imani aliyonayo sio sahihi. Wazazi wake wanakuona wewe ni kafiri, na wazazi wako wanaona umeoa/umeolewa na mtu asiye wa imani yako, utakuwa umetengeneza mgogoro wa kifamilia.

Yapo madhehebu tofauti tofauti na namna na yanavyoamini, yapo madhehebu misingi ya imani yao inafanana, na yapo misingi yao inatofautiana sana. Katika madhehebu haya kila kanisa linasimamia misingi yake, na washirika wamekua katika hiyo misingi, wapo hawawezi kukubali kuvunja misingi yao.

Wapo wanabatiza watoto, lakini wengine hilo suala halipo, wapo wanabatizwa na maji mengi na wengine maji machache, sina muda wa kutosha kukueleza nani yupo sahihi na nani hayupo sahihi ila ujue kama mmoja wenu hatakubaliana na hilo ujue umeshaingia kwenye mgogoro wa ndoa yako.

Hakikisha hili jambo hulipuuzi, kuna ndoa zimeingia kwenye shida kwa sababu baba anataka mtoto wake abatizwe akiwa mdogo na mama hataki mtoto wake abatizwe akiwa mtoto. Huu ni mfano tu, ipo mifano mingi sana hai inayotugusa kutokana na imani zetu.

Hakikisha mnakuwa pamoja katika imani kabla ya kuingia kwenye ndoa, na uwe na uhakika mwenzako au wewe hujamfuata mwenzako kwa sababu ya ndoa. Ninamaanisha kuwa isije ikawa mwenzako amekubali kuwa pamoja ili akuoe/umuoe baada ya hapo anarudi kwenye imani yake.

Hapa nazungumza na kijana ambaye ameokoka, usiseme mbona fulani walikutana wakiwa imani tofauti na wanaishi pamoja vizuri, usijilinganishe na yule ambaye hajaokoka wakakutana na mwenzake.

Imani ni moja ya msingi muhimu wa ndoa yako, ukipuuza hili utaona ndoa haikupi uhuru wa kumtumikia Mungu wako, unao uchaguzi sasa na sio kesho. Ukiona unapendwa sana na wa imani tofauti na yako, jiulize ni mpango wa Mungu au mapenzi ya Mungu muishi na huyo mwanamke/mwanaume?

Mwisho, kama una changamoto yeyote ya mahusiano au unapenda kufahamu kama jambo lolote kuhusu mahusiano, unaweza kuwasiliana nami kwa wasap namba +255759808081 au email; samsonaron0@gmail.com. Eleza changamoto yako kwa kina utapata majibu sahihi kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
+255759808081