
Ni kama swali rahisi na unaweza ukawa tayari una majibu yake, au ukawa huna uhakika na majibu yake.
Mara nyingi tumeona watu wakitukosea huwa wagumu kutuomba radhi, kwa kusingizia hawakuwa wanajua kama kufanya hivyo ni kosa.
Hata wewe mwenyewe huenda umekuwa mzito kuomba msamaha kwa kujipa moyo kwamba hukuwa unajua kama ni kosa/dhambi.
Huenda pia unajipa moyo kuwa yale uliyokosea mbele za Mungu bila kujua, hayo hutaweza kuhukumiwa nayo.
Je kweli hili la kufanya dhambi bila kukusudia linaweza likawa lipo kimaandiko? Huenda unajiuliza hili swali, nikupitishe kwenye Biblia uone.
Rejea: Na mtu awaye yote katika watu wa nchi akifanya dhambi pasipo kukusudia, kwa kufanya neno lo lote katika hayo ambayo BWANA alizuilia yasifanywe, naye akapata hatia; LAW. 4:27 SUV.
Unaona hilo andiko, linatupa ufahamu kwamba kuna dhambi ambazo tunafanya pasipo kukusudia.
Kufanya dhambi pasipo kujua kama umefanya, au pasipo kukusudia kama ungeweza kufanya dhambi kama hiyo. Hiyo haiwezi kuondoa nafasi ya kuomba msamaha mbele za Mungu.
Ndio maana huwa tunaomba toba mbele za Mungu kwa yale tunayokumbuka na tusiyoyakumbuka.
Yale tunayoyajua na tusiyoyajua, maana yapo mambo tunaweza tukamkosea Mungu bila kujua kama tunakosea.
Rejea: Tena kama mtu mmoja akifanya dhambi pasipo kujua, ndipo atasongeza mbuzi mmoja mke wa mwaka wa kwanza kuwa sadaka ya dhambi. Naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya huyo mtu akosaye, atakapofanya dhambi pasipo kujua, mbele za BWANA, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atasemehewa. HES. 15:27-28 SUV.
Uwe unajua au uwe hujui, fahamu kwamba unapaswa kutubia hayo yote uliyoyafanya.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com