Sio ajabu kuliona hili hasa kwenye jamii zetu za Kitanzania, mwanaume kulia machozi anaonekana kwenye jamii kama mtu wa kulialia hovyo na asiye na ukomavu wa mambo.

Kasumba hii imesababisha wanaume wengi kukaa na uchungu mwingi vifuani mwao huku wakijizuia kulia juu ya mambo yanayowasibu katika maisha yao.

Hili halijatokea tu, tangu mtu akiwa mtoto mdogo ameaminishwa kuwa wanaume huwa hawalii, inamlazimu mtoto kunyamaza tu.

Tunaweza kuona matokea mabaya ya wanaume wanaokaa na vitu vizito mioyoni mwao huku wakizuia hali ya kutolia, tofauti na wanawake wao hulia machozi.

Kupitia elimu hii, Yesu anatufundisha kuwa upo wakati wa kuumia, unapokutana na hali kama hiyo uzijizuie kupita kiasi bila kuonyesha hisia zako.

“Basi Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake, akasema, Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame. Yesu akalia machozi”, Yn 11:33‭-‬35 SUV.

Yesu anaonyesha huruma yake ya ndani kabisa kama aliyonayo Mungu kwa kuwasikitikia watu wake, kulia kwake machozi kunathibitishahili.

Mfano huu uwe faraja kwetu wana wa Mungu, hasa kwa wale wanaopitia hali ya huzuni, wajue Yesu yupo pamoja nao, ile shida waliyonayo, Yesu anaifahamu na atawasaidia.

Yesu anatuonea huruma ile ile aliyomwonea ndugu yake Lazaro, anatupenda kwa kiwango kile kile alichompenda Lazaro, hakuna chochote kilichopungua kwetu.

Fahamu kwamba katika kitabu hichi cha Yohana ambacho kimetupa maandiko haya, ndicho kitabu kinachosisitiza zaidi uungu wake kuliko kitabu chochote kile.

Huyu ndiye Yesu tunayemwamini, yaani Mungu na mwanadamu, aliye na uungu akilia machozi kama sisi wanadamu.

Tunapoenda kuhitimisha, elewa kwamba Mungu anao upendo wa ndani, na wa kihisia, ule wa huruma kwako na kwa wengine.

“Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako”, Lk 19:41‭-‬42 SUV.

Huu ndio upendo wa Mungu kwetu, tunahitaji kukaa naye kila wakati, uhusiano wetu na Mungu unapaswa kuwa bora kila siku.

Soma neno ukue kiroho
Kwetu kusoma biblia ni maisha
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081