Ukisoma katika kitabu cha Walawi 11:1-47 utaona Mungu akiwakataza wana wa Israel kula baadhi ya wanyama, Ndege, Wadudu, na kila kiumbe anayeishi kwenye maji.

Yule ambaye Mungu amemkataza ama yule ambaye hana sifa ambayo Mungu ameisema aliwe, hakupaswa kuliwa na mtu yeyote.

Kujitoa fahamu na kuanza kumla huko ni kujinasi mwenyewe, hili lilikuwa wazi bila kificho chochote. Maana ilikuwa ni sheria ambayo ilikuwa imewekwa.

Sasa wengi imekuwa kama utata, hasa tunapofika kwenye eneo la kula nyama ya nguruwe, maarufu kama kiti moto na majina mengi aliyebandikwa mnyama huyo.

Wapo samaki walikatazwa agano la kale, ambapo leo wengi tunakula na wengine wanaona kula ni dhambi. Wanaweza kukushangaa kweli kweli maana wana mistari ambayo wanaisimamia, hasa kwenye sura hii 11 ya kitabu cha Walawi.

Kipi cha kuchukua sasa kama mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni? Tuendelee kula vile vilivyokatazwa, au tuache kabisa kula, au tuendelee kubaki vile vile kutokula, au tuache misimamo yetu tuanze kula.

Ukisoma agano jipya kuhusu hili tunaweza kupata majibu ya maswali haya yote, hata kama utakuwa na MSIMAMO wa kula au KUTOKULA. Kupitia kujifunza hapa utaamua mwenyewe ubaki kundi lipi, yaani la kula au kutokula.

Ukisoma Biblia hasa agano jipya utaona hili suala la vyakula likiongelewa sana, kwa kuwa tupo agano lililo bora zaidi. Vizuri kulinganisha hii habari ya agano la kale na agano la sasa ambalo ni jipya.

Rejea: Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Marko 7:18-19.

Huyu ni Yesu mwenyewe akijibu swali la wanafunzi wake, hapa Yesu anatuambia wazi kupitia andiko hili Takatifu kuwa alivitakasa vyakula vyote.

Ukiendelea kujifunza kupitia maandiko mbalimbali utaona huu utata alikuwa nao pia PETRO, hakutaka kula chakula. Sikia alivyoambiwa na Mungu;

Rejea: Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Matendo ya Mitume 10:15.

Uzuri wa Mungu ni kwamba hatulazimishi katika hili na anatupa mwelekeo mzuri, hasa sisi ambao hatuoni tabu kutumia baadhi ya vitu ambavyo vinaonekana ni najisi.

Rejea: Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimhukumu mawazo yake. Warumi 14:1.

Vyakula vinaweza visiwe na shida yeyote kabisa ila kama unaona kwako ni najisi kula, hulazimishwi na mtu. Mtu mwelewa hapaswi kukulazimisha ule kile unaona kwako ni najisi.

Rejea: Kwa ajili ya chakula usiiharibu kazi ya Mungu. Kweli, vyote ni safi; bali ni vibaya kwa mtu alaye na kujikwaza. Ni vyema kutokula nyama wala kunywa divai wala kutenda neno lo lote ambalo kwa hilo ndugu yako hukwazwa. Warumi 14:20-21.

Kwanini sasa wale ambao wanakula wanakuwa hawana shida yeyote? Vizuri kufahamu hili kwa uthibitisho wa maandiko.

Rejea: Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki. Warumi 10:4.

Sheria iliyokuwepo kipindi cha Musa kwa wana wa Israel, Yesu Kristo alikuja kuwa mwisho wa hiyo sheria. Kwahiyo hakuna tena sheria kali za kukuzuia usile.

Torati alikuwa kiongozi wa kutuleta kwa Kristo, hili hatupaswi kulipuuza hata kidogo. Lakini huyo kiongozi hatuwezi kuendelea naye tena, maana tayari ameshatufikisha kwa Yesu Kristo.

Rejea: Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Wagalatia 3:24-26.

Usije ukahukumu watu wanaokula vyakula ambavyo vinaonekana ni najisi kwa mjibu wa Walawi 11, hatuko tena chini ya sheria.

Ruksa kula chakula au nyama ambayo unaona haina madhara kwako, na ikiwa yupo aliyemchanga katika hili. Labda anaona kula nguruwe ni dhambi, maandiko yanatusihi tusile mbele yake.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081